Watumishi Seka ya Ardhi watakiwa kutokuwa chanzo cha migogoro ya ardhi

NA MUNIR SHEMWETA
WANMM

KATIBU Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amewataka watumishi wa sekta ya ardhi kutokuwa chanzo cha migogoro ya ardhi na badala yake wawe wasuluhishi wa migogoro hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga akiangalia eneo itakapojengwa Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Tabora wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi pamoja na kuzungumza na watumishi wa sekta ya ardhi mkoani Tabora tarehe 9 Februari 2024.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

Aidha, amewataka watumishi wa sekta hiyo kufanya kazi kwa uadilifu na weledi katika kutimiza majukumu yao bila kusahau kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na taratibu.

Mhandisi Sanga ametoa kauli hiyo tarehe 9 Februari 2024 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi pamoja na kuzungumza na watumishi wa sekta ya ardhi mkoani Tabora.

Vile vile, kiongozi huyo alikagua miradi inayotekelezwa na Chuo Cha ardhi Tabora (ARITA) pamoja na kujadili changamoto zinazokikabili chuo hicho.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga akikagua majalada alipotembelea masijala ya ardhi ya Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tabora tarehe 9 Februari 2024. Kulia ni Kamishna wa Ardhi mkoa wa Tabora Husein Sadick.

Amewaasa watumishi hao wa sekta ya ardhi kuhakikisha kuwa, wanatoa majibu yenye uhakika kwa wateja na sio kuwazungusha pale wanapohitaji huduma za ardhi.

"Mhakikishe mnatoa majawabu ya uhakika kwa wananchi badala ya kuwapiga danadana na kuwazungusha bila sababu. Mwananchi ajisikie kuwa kuhudumiwa vizuri katika sekta ya ardhi siyo anasa bali ni haki yake,"alisema Mhandisi Sanga.

Aidha, amewataka watumishi hao kujenga tabia ya kuonyana wenyewe kwa wenyewe pindi mmoja wao anapokwenda kinyume na kanuni za utumishi wa umma.

Akigeukia suala la kodi ya ardhi, mhandisi Sanga amesisitiza suala la ukusanyaji mapato kupitia kodi ya pango la ardhi na kuwataka makamishna wa ardhi wasaidizi kote nchini kulisimamia jambo hilo kikamilifu kwa kuweka mikakati madhubuti.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga akioneshwa sehemu ya mradi wa jengo la maktaba ya Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) na Mkuu wa Chuo hicho Biseko Musiba wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi pamoja na kuzungumza na watumishi wa sekta ya ardhi mkoani Tabora tarehe 9 Februari 2024.

Kwa upande wa Chuo cha Ardhi Tabora, ameutaka uongozi wa Chuo hicho kukaa na kutafakari ni namna gani watakuja na mipango ya maboresho ya kimitaala na miundombinu ya chuo ili kiweze kujiendesha katika hali ya ushindani na vyuo vingine.

Ameweka wazi kuwa, ataunda timu ndogo itakayokuwa na jukumu la kukaa na kutafakari na hatimaye kuja na mapendekezo ya kuboresha chuo hicho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news