DODOMA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama ameipongeza Serikali kwa kuboresha maslahi ya watumishi nchini kwa lengo la kuinua hali zao za kiuchumi ili waweze kumudu gharama za maisha na kutekeleza majukumu yako katika mazigira rafiki.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa viongozi wa TUGHE uliomtembelea ofisi kwake bungeni Jijini Dodoma.
Waziri Jenista ameyasema hayo wakati akizungumza na ujumbe wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) ofisini kwake bungeni jijini Dodoma ukiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho,Dkt. Jane Madete ambapo alisema ni dhamira ya Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha watumishi maslahi yao yanaboreshwa.
Amesema kuwa, kwa kipindi cha muda mfupi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali, zahanati na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba katika maeneo mbalimbali nchini.
“Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa kiongozi mahiri ndani ya kipindi kifupi sisi wenyewe ni mashahidi ametekeleza miradi mikubwa sana ya maendeleo na amekuwa mstari wa mbele kuboresha miundo mbinu ya wafanyakazi ili muweze kutoa huduma vizuri na anawapenda sana wafanyakazi,”alisema Mhe. Jenista.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na ujumbe wa TUGHE uliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa TUGHE,Dkt. Jane Madete na Mwenyekiti wa Kamati ya wanawake TUGHE Taifa Bi, Catherine Katele Ofisini kwake Bungeni Jijijni Dodoma.
Pia, Waziri Jenista ameupongeza uongozi wa TUGHE kwa kuendelea kuimarisha chama hicho kikizingatia misingi na katiba ya chama huku akihimiza ushirikiano baina yao hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku na kuchochea maendeleo ya Taifa.
“Niwapongeze kwa ziara yenu leo, mmeendelea kusimamia katiba ya chama, kujenga ustahimilivu , kuvumiliana na kujenga umoja ili kuimarisha chama kwahiyo kwa niaba ya Seraikali ninawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuwaweka watumishi wote pamoja kwa amani,”alipongeza.
Aidha, aliwasisitiza kuendelea kuzingatia sheria na taratibu za utumishi wa umma pamoja na kufanya kazi kwa moyo wa kujitolea na ubinifu kwa manufaa ya Nchi nzima na wananchi kwa ujumla.
Makamu Mwenyekiti wa TUGHE Dkt. Jane Madete akimkabidhi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe Jenista Mhagama tuzo ya kutambua mchango wake kwa wafanyakazi.
“Nitoe wito endeleni kushikimana, kukifanya chama chenu kuheshimika hali itakayovutia kupata wanachama wengi zaidi . Pia mzingatie sheria za Nchi pamoja na kuwasisitiza wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na kuwa tayari kuelezea mafanikio yenu na kuishauri Serikali maeneo ambayo inaweza kuboresha,”alieleza.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa TUGHE Dkt. Jane Madete alibanisha kwamba lengo la ziara yao kutambua mchango wake mkubwa katika Chama hicho pamoja na kujadili kwa pamoja namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi na kuipongeza Serikali katika uboreshaji wa huduma za wananchi.
“Ujio wetu huu ni kupongeza Serikali kwa namna inavyoboresha huduma kwa wananchi husudani sekta ya afya tumeona hospitali nyingi zimejengwa kuanzia katika vijini hadi mikoa na tumemshauri Mhe. Waziri waone umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu ya hospitali zilizojengwa kwa muda mrefu ili kurahisisha utoaji wa huduma ya afya kwa wananchi,”alieleza Dkt. Jane.
Mbunge wa vitu maalumu anayewakilisha wafanyakazi Mhe, Janejelly Ntate akizungumza wakati wa Ujumbe wa Viongozi wa TUGHE ulipomtembelea Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu ) Mhe Jenista Mhagama Ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma.
Aidha, Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha wafanyakazi Mhe. Janejelly Ntate aliwasihi wafanyakazi kuendelea kuiamini Serikali ya Awamu ya Sita kwani imeendelea kutikiza ahadi zake kwa vitendo na kuwataka wafanyakazi kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.
Tags
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE)
Habari
TUGHE
TUGHE Tanzania