Waziri Mkuu aitaka WMA kusimamia vema sheria

DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wa Wakala wa Vipimo (WMA), wasimamie vema sheria ya vipimo na kanuni zake kwa kukagua na kuhakiki mara kwa mara vipimo vinavyotumika katika sekta mbalimbali ikiwemo ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa na ufungashaji sahihi wa mazao ya kilimo.
“Watumishi wote wa Wakala wa Vipimo kumbukeni kuwa taasisi yenu imepewa wajibu wa kumlinda mlaji, muuzaji na mnunuzi kwa kuhakikisha kile kinachonunuliwa au kuuzwa kinakuwa sawa kabisa na vipimo vilivyoainishwa. Hivyo, kila mmoja atimize wajibu wake huo kwa jamii.”

Ametoa maagizo hayo Jumanne, Februari 6, 2024 baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi ya Makao Makuu ya WMA katika eneo la Medeli jijini Dodoma. Mheshimiwa Majaliwa ameweka jiwe hilo la msingi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Pia, Waziri Mkuu ameuelekeza wakala huo uweke utaratibu mahsusi wa kuthibiti wa masuala ya ufungashaji wa bidhaa usiozingatia vipimo sahihi (lumbesa). “Kero hii imekuwa ya muda mrefu ni lazima mhakikishe mnaondoa malalamiko ya wakulima ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo wahanga wa kudhulumiwa kwa kulazimishwa kufungasha kwenye ujazo ambao haukubaliki kisheria.”

Mbali na maelekezo hayo kwa vongozi wa WMA, pia Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwataka wafanyabiashara wote nchini wazingatie utaratibu na kanuni za vipimo vilivyowekwa na Serikali na waache mtindo wa kuchezesha mizani bali watumie vipimo vya haki.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji amesema ujenzi wa jengo hilo utakaogharimu shilingi bilioni 6.17 hadi kukamilika kwake ni sehemu ya juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uboreshaji wa mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma.

Waziri huyo amesema kuwa mradi huo unaotekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani unakwenda sambamba na ujenzi wa ofisi nyingine za wakala huo katika mikoa ambayo haina ofisi ili kuendelea kuboresha huduma mbalimbali zinazotolewa nchini kote.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Mhandisi Stella Kahwa alisema ujenzi wa mradi huo unaojengwa kwa kipindi cha miezi 30 ulianza rasmi tarehe 01 Julai, 2022 na utakamilika tarehe 25 Januari, 2025, umefikia asilimia 70.36. 

“Jengo hili la ghorofa tano, linajumuisha vyumba vya ofisi 60, maabara, kumbi za mikutano na kantini”.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news