MARA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma ambapo amesema ni faraja kuona Serikali ikiendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo uwanja huo.
Amesema kuwa, maamuzi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo ni ya kuungwa mkono kwa ni fursa kwa wafanyabiashara na wakazi wa maeneo hayo.
“Uwanja huu utaleta fursa kwa wafanyabiashara na wakazi wa mkoa huu na wilaya zake, kwasababu itawezesha kuendelea kukua kwa sekta ya utalii kwenye mkoa huu ambao kuna mbuga ya Serengeti.”
Amesema kuwa, ujenzi wa uwanja huo kama ilivyo kwa ujenzi wa viwanja vingine duniani, viwango na umakini utazingatiwa.
“Kwa kuwa TANROADS ndio mnasimamia hili sisi hatuna mashaka, tunaamini kazi hii inaendelea, awamu za ulipaji wa fedha hizo hazina mashaka, mkandarasi atalipwa ili akamilishe kazi hii kwa wakati.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Wana-Mara kutumia fursa ya ujenzi wa uwanja huo ikiwemo ujenzi wa hoteli.“Jengeni hoteli za kisasa kuanzia nyota tano, nne na kuendelea.”
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amewataka walioajiriwa katika mradi huo kufanya kazi hiyo kwa weledi ili ujenzi uwe wa viwango.
“Nimeambiwa zaidi ya asilimia 80 walioajiriwa hapa ni watanzania, ninyi ni wasaidizi wakusimamia viwango, wakati wote hakikisheni suala la viwango vinavyosisitizwa na Mainjinia linapewa kipaumbele.”
Ujenzi wa uwanja huo ambao umefikia asilimia 55 utagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 35 na ukarabati utahusiaha Ukarabati wa njia ya kuruka na kutua ndege (runway) yenye urefu wa mita 1,705 na upana mita 30 kwa kiwango cha lami, ukarabati wa njia ya kiungio (taxiway) kwa kiwango cha lami, Ukarabati wa eneo la maegesho ya ndege (Apron) kwa kiwango cha lami.