Waziri Mkuu akemea wizi kwenye miradi ya umma

MARA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekemea vitendo vya wizi na uzembe kwenye usimamizi wa ujenzi wa miradi ya umma nchini.

“Tumeshaibiwa mifuko zaidi ya 600 kwenye ujenzi wa shule hii ya sekondari ya wasichana ya Mara, hakuna usimamizi, hakuna anayejali, mmengeanza kuchukua hatua ninyi wenyewe Halmashauri kabla hata Mkuu wa Mkoa hajaja."
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua maabara katika shule ya sekondari ya wasichana ya Mara, kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule hiyo Februari 26, 2024. Mheshimiwa Majaliwa amewataka wajenzi wa shule hiyo kufanya kazi usiku na mchana ili iweze kukamilika ifikapo julai 2024 na ianze kupokea wanafunzi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Februari 26, 2024 alipokagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mara Kata ya Buramba wilaya ya Bunda mkoani Mara

“Kwa nini Muentertain wizi? Watu wanaiba mara ya kwanza, mara ya pili mmeshindwa kuchukua hatua za kuwadhibiti wasirudie tena?, Halafu si hapa tuu, hata hospitali ya wilaya ina matatizo mengi, mmeshang’oa na milango iliyofungwa, mmeshaiba na vifaa tiba ikiwemo mashine ya X-Ray, sasa nyie Bunda mkoje?” alihoji Mheshimiwa Majaliwa.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa haridhishwi na utendaji kazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa kukosa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dkt. Vicent Naano adhibiti vitendo vya wizi kwenye Halmashauri hiyo. “Halmashauri hii fedha za Serikali zinakuja nyingi sana, na si lazima aje Mkuu wa Mkoa, wewe una Kamati ya Usalama, uzembe ni mwingi, hatuwezi kukubaliana nalo hili.”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania kuwa walinzi wa miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ili iweze kukamilika kwa wakati na kutoa huduma kama ilivyokusudiwa na Rais Dkt. Samia.

“Wananchi ni muhimu kutoa taarifa ili kuzilinda rasilimali n fedha na miradi, iwe ya shule, afya, elimu hata barabara hili pia ni jukumu lenu, mkiona dalili za wizi kwenye miradi yetu toeni taarifa, hatuwezi kuwavumilia wezi hawa, wanakwamisha juhudi za Rais wetu kuleta maendeleo.”

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mara, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wajenzi wa shule hiyo kufanya kazi usiku na mchana ili iweze kukamilika ifikapo Julai 2024 na ianze kupokea wanafunzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news