NA FRESHA KINASA
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema kuwa,Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo ni kiongozi mwenye heshima na mahiri hapa nchini hivyo wananchi wa jimbo hilo waendelee kumpa ushirikiano na kumwamini katika utendaji kazi wake wa kuwatumikia kuwaletea maendeleo.
Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo Februari 29, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa (Bwai Kumusoma) katika mkutano wa hadhara akiwa katika siku ya tano ya ziara yake Mkoani humo aliyoianza kuanzia Februari 25, 2024, hadi Februari 29, 2024.
Kutokana na umahiri wa Prof. Muhongo amewataka wananchi wa jimbo hilo kutambua kwamba wana kiongozi sahihi wa kuzifikisha serikalini changamoto zao zote na Serikali ikazipatia ufumbuzi kwa ajili ya maendeleo yao.
"Niwaombe wananchi muendelee kumuamini Prof. Muhongo amekuwa akipambana kwa ajili yenu ni kiongozi makini na mahiri serikali imeendelea kuleta fedha na kujenga miradi mingi kutokana na juhudi ambazo amekuwa akizionesha kwa kuomba fedha za miradi. Mengi ameyaandika kwenye kitabu akielezea yaliyofanyika," amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wananchi wa Jimbo la Musoma kujishughulisha na shughuli za uvuvi wa kisasa kwa kuunda umoja wa Wavuvi ambao utawasaidia kufanya uvuvi wa kisasa utakaowaingia kipato na kukuza uchumi wao.
"Undeni vikundi mzalishe samaki wengi, hii ni fursa kubwa kwenu wananchi wa Musoma, nawashawishi kwamba mnatakiwa kuvua samaki kwani uvuvi ni pesa, nimewambia Mkurugenzi miwe na soko la uhakika la samaki ili bei iwe moja na kusitokee mvuvi wa kuonewa.
"Mnaweza kuandika andiko au mkatumia fedha za ndani ili watu wapate soko la uhakika,"amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha,Waziri Mkuu Majaliwa amekemea vikali kitendo cha uvuvi haramu ndani ya ziwa Victoria ili kulinda mazalia ya samaki. Huku akimtaka Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Musoma kuwa na utaratibu wa kufanya doria maeneo ya fukwe kwa kudhibiti vitendo vya uvuvi harakamu akishirikiana na Wananchi na watendaji wa Vijiji.
Aidha,Waziri Mkuu Majaliwa, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Kuhakikisha inasimamia ujenzi wa Zahanati katika Kila Kijiji Wilayani Musoma ili Wananchi wapate huduma huku akisema Serikali itaendelea kutoa fedha za ujenzi wa vituo vya afya zaidi Wilayani humo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo amemshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kusema kwamba, Serikali ya Dkt. Samia Hassan imekuwa ikitoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo jimboni humo.
Huku pia akimkabidhi Waziri Mkuu vitabu vinavyoonesha utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi kwa mafanikio makubwa jimboni humo.
Waziri Mkuu Majaliwa amehitimisha ziara yake mkoani Mara Februari 29, 2024 kwa kuhutubia Wananchi wa Manispaa ya Musoma katika Uwanja wa shule ya Sekondari Mara uliopo Manispaa ya Musoma. Ambapo amewataka Viongozi wa Mkoa wa Mara kuwajibika kutatua Kero za wananchi.
Safi profesa Muhongo Kwa Maendeleo,
ReplyDelete