NA GODFREY NNKO
WAZIRI Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Edward Lowassa amefariki dunia, akiwa anapatiwa matibabu jijini Dar es Salaam.
Lowassa alikuwa Waziri Mkuu wa Tisa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipokea nafasi hiyo kutoka kwa Mheshimiwa Fredrick Tluway Sumaye.
Alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia Desemba 30, 2005 hadi Februari 7, 2008 alipojiuzulu na hatimaye kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri. Alikifuatiwa na Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda.
Tangazo la kifo cha Lowassa limetangazwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango.
Katika tangazo fupi alilolitoa kupitia televisheni ya taifa, Mpango amesema kuwa Lowassa amefikwa na umauti katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameeleza kupokea kwa mshutuko taarifa za kifo cha Edward Lowassa,
"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa.
"Mheshimiwa Lowassa ameitumikia nchi yetu katika nafasi mbalimbali kwa zaidi ya miaka 35, akianzia ushiriki wake katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge, Waziri katika wizara mbalimbali na Waziri Mkuu.
"Tumempoteza kiongozi mahiri, aliyejituma na kujitoa kwa nchi yetu. Natoa pole kwa mjane, Mama Regina Lowassa, watoto (Mheshimiwa Mbunge wa Monduli, Fredrick Lowassa na wadogo zako), ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mzito.
"Katika mawasiliano yangu na familia, nimewaeleza kuwa kama taifa tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu, na kamwe wasiache kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutafakari neno lake, hasa Kitabu cha Ayubu 1:21.Mwenyezi Mungu amweke mahali pema. Amina,"amefafanua Rais Dkt.Samia.
Edward Ngoyai Lowassa |
---|
|
| Mbunge |
Bunge la | Tanzania |
Jimbo la uchaguzi | Monduli (Arusha) |
Tarehe ya kuzaliwa | 26 Agosti 1953 |
Tarehe ya kifo | 10 Februari 2024 |
Chama | CCM (tangu 01/03/19) |
Tar. ya kuingia bunge | tangu 1990 |
Alirudishwa mwaka | 2005 |
| Waziri Mkuu wa Tanzania |
Alingia ofisini | 2005 |
Alitanguliwa na | Frederick Sumaye |
Dini | Mkristo |
Elimu yake | Chuo Kikuu |
Digrii anazoshika | MA (Development Studies) University of Bath (Uing.) |
Kazi | mwanasiasa |
Nafasi alizowahi kuhudumu kama mtumishi wa umma kwa nyakati tofauti nchini;Nafasi | Mwaka |
Waziri Mkuu | 2005–2008 |
Mbunge wa Jimbo la Monduli | 1990–2015 |
Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo | 2000–2005 |
Waziri wa Nchi, Mazingira na Mapambano dhidi ya Umasikini (Ofisi ya Makamu wa Rais) | 1997–2000 |
Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi | 1993–1995 |
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (Haki na Masuala ya Bunge) | 1990–1993 |
Mkurugenzi Mtendaji wa Arusha International Conference Centre (AICC) | 1989–1990 |
Aidha, mwaka 2014 Edward Lowassa alisimamishwa na Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kushtakiwa kwamba aliwahi kuanzisha kampeni ya kuwa mgombea wa urais kabla ya kipindi kilichokubaliwa na chama hicho
Mei 2015,alianzisha kampeni yake rasmi,lakini kamati kuu ya CCM ilimuondoa katika orodha ya majina yaliyopelekwa kwa uteuzi ndani ya chama.
Lowassa aliondoka CCM na Julai 28, 2015 alijunga rasmi na chama cha upinzani cha CHADEMA.
Siku chache baadaye aliteuliwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CHADEMA mnamo Oktoba 2015.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi alishindwa kwa kupata asilimia 39.97 za kura zote na mgombea wa CCM, ambaye kwa sasa ni marehemu, Dkt. John Pombe Magufuli aliyepata asilimia 58.46 ya kura.
Licha ya kushindwa kutimiza ndoto ya urais, Lowassa aliendelea kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA.
Ingawa, Januari 2018 alifanya mazungumzo na Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, bila kujua kilichojadiliwa Machi Mosi,2019 alirejea tena Chama Cha Mapinduzi.