DODOMA-Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo ameongoza kikao baina ya Wizara na Uongozi wa Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Ltd kujadili Maendeleo ya Utekelezaji wa Mradi wa Uchimbaji na Uchenjuaji wa Madini ya Nikeli.
Kikao hicho kilichojadili kwa kina masuala mbalimbali yanayohusu uendelezaji wa Mradi huo ikiwemo mazingira, ulipaji fidia, upatikanaji wa nishati ya umeme, miundombinu ya barabara pamoja na changamoto zinazokabili utekelezaji wake, kimefanyika Februari 15, 2024 jijini Dodoma huku baadhi ya washiriki kutoka kampuni ya Tembo Nickel wakishiriki kwa njia ya mtandao.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Tembo Nickel Benedict Busunzu ameiomba Wizara kusaidia kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo katika Mradi huo ili kutokukwamisha utekelezaji wake. Busunzu amezitaja kadhaa kuwa ni pamoja miundombinu ya barabara, reli, pamoja na masuala ya kikodi.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kila mara kuwa sikivu kwa kampuni hiyo kila mara inapohitaji kufanya hivyo na kupata mrejesho wa masuala mbalimbali yanayowasilishwa Serikalini na kuongeza kwamba, wanapongeza utaratibu uliowekwa na wizara kukutana na wawekezaji kila robo mwaka.
Masuala mengine katika taarifa ya kampuni hiyo yamegusia miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwa jamii inayozunguka mradi huo (Local content na CSR) kwenye afya na elimu ambapo mwaka huu wa 2024 kampuni ya Tembo Nickel itakabidhi miradi ya thamani ya Tsh milioni 256 kwa halmashauri ya Ngara.
Akizungumzia masuala ya ununuzi na shughuli za utoaji huduma migodini, Afisa Mkuu wa Masuala ya Fedha, Frank Kilua amesema kwa mwaka 2023, kiasi cha fedha kilichotumika katika eneo la Ngara pekee thamani ya manunuzi hayo ilifikia Tsh bilioni 1.7, kwa Tanzania nzima thamani ya manunuzi ilifikia kiasi cha Tsh bilioni 67.8, manunuzi ya nje shilingi bilioni 1.46 na hivyo kufanya kiasi cha thamani ya manunuzi yote kwa mradi huo kufikia shilingi bilioni 71.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Mbibo amewahakikishia wawekezaji hao kuwa wizara itahakikisha inayafanyia kazi masuala yote ambayo yapo katika ngazi ya Wizara na yale yaliyo katika mamlaka nyingine Wizara itayafuatilia ili kuhakikisha Mradi huo unatekelezwa kama ilivyopangwa.
Mradi wa Kabanga Nickel wa uchimbaji madini na uchakataji wa madini ya nikeli ni Mradi unaotarajiwa kuwa wa aina yake si, Tanzania tu bali duniani kutokana na uhitaji mkubwa wa madini hayo. Madini ya nikeli ya Kabanga yanatajwa kuwa kati ya madini ya Nikeli yenye ubora wa kiwango cha juu duniani.
Kwa Tanzania, shughuli za uchimbaji wa madini hayo zitafanyika katika eneo la Kabanga, Wilayani Ngara Mkoa wa Kagera ambapo zaidi ya hekta 4,000 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi huo unaotarajiwa kuanza uzalishaji ifikapo mwishoni mwa mwaka 2026. Kwa upande wa Kiwanda cha kuchenjua madini hayo kitajengwa katika Wilayani kahama Mkoa wa Shinyanga.
Katika mradi huo, Serikali ina umiliki wa hisa za asilimia 16 zisizohamishika.