RUKWA-Kikao cha kawaida cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Rukwa (RCC) kimefanyika Februari 13,2024 katika ukumbi wa RDC ulioko ofisi ya Mkuu wa mkoa huo.
Kikao hicho kimepokea taarifa mbalimbali zikiwemo taarifa za mapato kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), taarifa za makusanyo ya mapato kwa Halmashauri za Wilaya za Sumbawanga, Nkasi, Kalambo na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.
Taarifa zingine ni taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, taarifa za maendeleo ya sekta ya maji, taarifa ya usambazaji wa umeme vijijini, taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa lishe na rasimu ya mpango na bajeti ya Mwaka 2024/25 kwa Mkoa wa Rukwa.
Washiriki wa kikao hicho wameshauri pamoja na masuala mengine muhimu, mipango na bajeti ya 2024/25 izingatie na kutoa kipaumbele kwa ukamilishaji wa miradi ya maendeleo ambayo haijakamilika.
Wameshauri pia juu ya kuimarishwa kwa usimamizi kwa Mkandarasi anayesambaza umeme vijijini.
Suala la lishe bora na kamili limejitokeza pia likiwa miongoni mwa masuala muhimu yaliyojadiliwa katika kikao hicho.