DAR ES SALAAM-Klabu ya Yanga (Young Africans Sports Club) ya jijini Dar es Salaam imeibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria.
Ni katika mchezo wa Kundi D Ligi ya Mabingwa barani Afrika ambao umepigwa usiku huu.
Mtanange huo wa nguvu umepigwa leo Februari 24,2024 katika Dimba la Benjamin Mkapa katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Mabao hayo yamewekwa nyavuni na Mudathir Yahya Abbas dakika ya 43, Stephane Aziz Ki dakika ya 47.
Mengine yamefungwa na Kennedy Musonda dakika ya 48 na Joseph Guede Gnadou dakika ya 84 ya kipindi cha pili cha mchezo huo.
Chini ya Kocha Miguel Ángel Gamondi, kwa matokeo hayo Yanga inafikisha alama nane na kusogea nafasi ya pili ikiwa ni nyuma ya mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri baada ya wote kucheza mechi tano.
Aidha,CR Belouizdad wanabaki na alama zao tano mbele ya Medeama SC ya Ghana yenye alama nne inayoshika mkia baada ya wote kucheza mechi tano.
Katika hatua nyingine Yanga SC kwa matokeo hayo imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali.
Wenyeji hao walikuwa wanahitaji ushindi wa mabao 4-0 kwenye mchezo huo ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali, kwani mechi ijayo ambayo watacheza na Al Ahly hata kama akifungwa basi atakuwa amebaki na alama nane.