ZANZIBAR-Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar (ZIAAT), CPA Ame Burhan Shadhil tarehe 13 Febuari, 2024 ameongoza Mkutano kati ya Uongozi wa ZIAAT na Wahasibu na Wakaguzi wa Umma waliothibitishwa.
Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni Mjini, Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji ameeleza kuwa, lengo kuu la ZIAAT ni kusimamia utoaji wa huduma bora kwa wanachama wake pamoja na kusimamia maadili na Uadilifu katika Taaluma ya Uhasibu.
Naye Afisa Mwandamizi wa ZIAAT, CPA Dkt. Khamis M. Khamis amesema kuwa, kupitia mafunzo yatakayotolewa na ZIAAT yatawasaidia Wahasibu na Wakaguzi kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa na usahihi.
Aidha, CPA Riziki Faki kutoka Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ameeleza kuwa, kupitia mkutano huo wamefahamu kuna chombo kinachosimamia Taaluma ya Uhasibu, hivyo amewaomba Wahasibu na Wakaguzi wote wenye CPA kuchukua fomu za usajili ili watambuliwe kisheria.