MAPUTO-Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji,Mheshimiwa Phaustine Kasike amekutana na Prof.Armindo Tiago ambaye ni Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Msumbiji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji imeeleza kuwa, viongozi hao wamekutana leo Machi 20,2024 kwenye ofisi za wizara ya hiyo zilizopo jijini Maputo.
Wakati wa mkutano huo, viongozi hao wawili walizungumza masuala mbalimbali ya ushirikiano katika Sekta ya Afya ikiwemo pendekezo la kusainiwa Hati ya Makubaliano (MoU) itakayowezesha Tanzania kuuza madawa na vifaa tiba nchini Msumbiji
Viongozi hao, pia walizungumzia pendekezo la Tanzania la kutuma timu ya wataalam wa afya watakaoweka kambi nchini Msumbiji kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wenye matatizo ya moyo.