DAR ES SALAAM-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha kikao kazi cha majadiliano na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kuhusu mwenendo wa sekta ya huduma ndogo za fedha nchini.
Aidha,kikao hicho kilichoongozwa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sekta za Fedha, Bw. Sadati Musa, kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Ustawi wa Huduma Jumuishi ya Fedha, Bw. Kennedy Komba, kilihusisha pia watendaji kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya Mkoa wa Dar es Salaam na halmashauri za Kigamboni na Ilala.
Kikao hicho kililenga kujenga uelewa wa namna Benki Kuu inavyosimamia sekta ya huduma ndogo za fedha pamoja na majukumu ya OR-TAMISEMI katika masuala ya kusimamia na kuratibu sekta hiyo.
Pia, wadau hao walijadili changamoto mbalimbali zinazowakabili katika usimamizi na uratibu wa sekta hiyo pamoja na kupendekeza namna ya kutatua changamoto hizo ili kuongeza usalama, uimara pamoja na ustawi wa huduma jumuishi za fedha.