BoT yazitaka hoteli kuwa na leseni huduma fedha za kigeni ifikapo Julai 1

ZANZIBAR-Benki Kuu ya Tanzania imezihimiza hoteli kuhakikisha zinapata leseni ya kutoa huduma za fedha za kigeni ifikapo tarehe 1 Julai 2024 ili kutokomeza uuzaji holela wa fedha za kigeni nchini.
Haya yamesemwa leo Machi 22, 2024 na Gavana wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba, alipokutana na wamiliki na waendeshaji wa hoteli za kitalii Zanzibar katika Ofisi za Makao Makuu Ndogo ya Benki Zanzibar.

Amesema marekebisho ya Kanuni za Maduka ya Kubadilishia Fedha za Kigeni ya mwaka 2023 yanatoa fursa kwa hoteli za kitalii kupata leseni ya kutoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni kwa wateja wao.
“Tumezijulisha hoteli ifikapo tarehe 1 mwezi wa saba tutapita tuone kama hoteli zote zimeanza kutoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni ili kurahisisha biashara zao na kuwawezesha kutoa huduma ya fedha za kigeni kwa wateja wao. Watakuwa na wajibu wa kutoa takwimu na taarifa sahihi za miamala waliyopokea na kwenda kuziweka kwenye mabenki,"amesema.

Gavana Tutuba alisema kuwa Benki Kuu ya Tanzania ilipitia Kanuni za Maduka ya Kubadilishia Fedha za Kigeni ya mwaka 2019 kwa lengo la kupunguza baadhi ya mahitaji ili kuhamasisha uwekezaji katika biashara hiyo.
Aliwaeleza kuwa marekebisho ya Kanuni hizi yamepunguza kiwango cha mtaji kinachohitajika ili kufungua maduka haya na pia alisema kuwa marekebisho hayo yameziruhusu hoteli zinazoanzia nyota tatu hadi tano kuanza kutoa huduma za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni.

“Katika Kanuni za mwaka 2023 kiwango cha chini cha mtaji cha kinachotakiwa kisheria kimepunguzwa, ambapo huko nyuma ilikuwa ni changamoto kwa wawekezaji wengi nchini,” alisema.

Pia, amesisitiza kuwa BoT itaendelea kusimamia upatikanaji wa fedha za kigeni nchini ili kuwezesha ufanyaji biashara.
“Uchumi unaendelea kufunguka na vile vihatarishi vilivyokuwa kwenye uchumi wa dunia vinazidi kupungua. Sisi tutaendelea kusimamia fedha za kigeni ziendelee kupatikana na zisaidie biashara halali.’’

Kwa upande wao, wamiliki wa hoteli hizo wameishukuru Benki Kuu kwa kuitisha kikao hicho na wameahidi kuendelea kuishauri katika mambo mbalimbali na kuibua changamoto zilizopo katika sekta kwa lengo la kuzipatia utatuzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news