MOROGORO-Serikali imesema itaendelea kuhakikisha inawezesha mazingira bora na rafiki kwa vijana wabunifu kwa kutoa mikopo, ajira na kuwapa fursa mbalimbali kwa kutumia taaluma vyema katika kung’amua fursa katika jamii.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. William Mwegoha wakipata maelezo kutoka kwa wajasiriamali walioshiriki katika Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali mwishoni mwa wiki.
Hayo yamezungumzwa katika Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali, na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli, kwa hadhira iliyohudhuria tukio hilo Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro mwishoni mwa wiki.
Mhe. Nguli amesema kuna dhana kuwa wasomi wengi wanahisi Serikali haiwasaidii kupata ajira lakini si kweli na kuwataka wasomi kutumia taaluma zao kubuni bunifu mbalimbali, kuendana na soko la ajira na kubadilisha mtazamo uliopo wa kusubiri ajira za Serikali kwani nguvu, fikra na mtazamo wa kujiajiri ndio unahitajika.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli akizungumza na Makamu Mkuu Wa Chuo Prof. William Mwegoha mara baada ya kutembelea Chuo Kikuu Mzumbe hivi karibuni.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Judith Nguli amesema Serikali itaendelea kuhakikisha inawezesha mazingira bora na rafiki kwa vijana wabunifu kwa kutoa mikopo, ajira na kuwapa fursa mbalimbali kama alivyoelekeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akiwataka vijana kutumia taaluma vyema katika kung’amua fursa katika jamii.“Leo limefanyika tukio kubwa katika historia, sisi kama Serikali nichukue nafasi hii kuwahidi wasomi kuwa watapata ushirikiano wa kutosha, tunafursa nyingi Serikalini, niseme dunia imebadilika, mazingira yamebadilika, tunafundishwa ili taaluma zetu tukazitumie katika maisha ya kawaida, nawaomba sana vijana tuwaze nje ya box kwa kuwa na mawazo ya ubunifu na sisi kama Serikali tutaunga mkono mawazo hayo,” amesema Mhe. Mhe. Nguli.
Aidha, ametoa pongezi kwa Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuandaa kambi ya kuwakutanisha wanafunzi wabunifu na wajasiriamali. Ametumia nafasi hiyo pia kuwakabidhi tuzo mbalimbali wanafunzi, wafanyakazi na wadau walioalikwa kushiriki tukio hilo, baada ya kupitia katika mabanda ya wajasiriamali na kuona mawasilisho ya bunifu zilizowasilishwa na wanafunzi.
Kwa shindano la mawazo ya biashara; mshindi wa kwanza amepata kitita cha Shilingi milioni moja, mshindi wa pili amepata laki saba na mshindi wa tatu amejinyakulia shilingi laki tatu.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Mzumbe Prof. William Mwegoha amesema kupitia Mradi Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi( HEET) Chuo kimepata Dola za Kimarekani milioni 21, kuendeleza ili Chuo ambapo sehemu ya fedha hizo zitatumika kujenga Kituo cha Kukuzia Ubunifu na Vipaji vya Wanafunzi Wajasiriamali ili kuwapa fursa zaidi wanafunzi na wafanyakazi kufanya shughuli za kibunifu na ujasiriamali.
Prof. Mwegoha ameongeza kuwa kwa mwaka huu wa 2024,Chuo kimeongeza wanufaika na kambi ya ujasiriamali zaidi ya 20 kutoka nje ya Chuo wakilenga kujenga mahusiano mazuri na wadau pamoja na kutoa fursa kwa wanafunzi kupata uzoefu kutoka kwa makampuni makubwa.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na ushauri, Prof. Eliza Mwakasangula ametoa shukrani kwa wadau mbalimbali waliofanikisha Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali na kusisitiza kuwa Chuo kinaendelea kuweka mazingira wezeshi ya ubora wa kitaaluma.
Mambo yaliyofanyika Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali yanadhihirisha wazi kaulimbiu ya Chuo hicho: “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu."