MOROGORO-Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeitaka jumuiya ya Chuo Kikuu cha Mzumbe kuchangamkia fursa ya kurasimisha biashara zao ili ziweze kutambulika na kulindwa kisheria.
Hayo yamesemwa na Bi. Loy Mhando Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA wakati akiwasilisha mada kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu, juu ya umuhimu wa kurasimisha biashara katika Maadhimisho ya Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali 2024. Maadhimisho hayo yanayofanyika Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro kuanzia tarehe 20 hai 22 Machi 2024.
“Zipo faida nyingi zitokanazo na kurasimisha biashara ikiwemo, urahisi wa kufikiwa kwa huduma mbalimbali kwa kuwa kutawezesha kupata takwimu sahihi za biashara, vilevile biashara hizo zitatambulika kisheria. Vilevile, mfanyabishara ataweza kuweka hesabu vizuri na kuweza kupata huduma mbambali ikiwemo ikiwemo mikopo,”alisema Bi. Mhando.
Aidha,Bi. Mhando ameongeza kwa kusema kuwa, urasimishaji biashara utawezesha wafanyabiashara kulipa kodi ambayo itachangia katika kukuza uchumi wa taifa utakaowezesha ujenzi wa miundombinu ya kuwafikia wafanyabiashara sambamba na ujenzi wa masoko na uwekaji wa mazingira wezeshi ya biashara.


Maadhimisho hayo yaliyobeba Kauli Mbii isemayo “Kuzingatia Teknolojia Zinazoibukia na Njia Mpya za Kujifunza kwa ajili ya Ukuaji Endelevu”, yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 22 Machi, 2024. Kauli Mbiu hiyo inayolenga kuibua vipaji na mawazo bunifu ya wanafunzi wa Chuo hicho na pia kutoa nafasi kwa wafanyakazi na wanafunzi kuonesha ubunifu walionao.