DAR ES SALAAM-Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt.Emmanuel John Nchimbi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba, nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne Vera.
Katika mazungumzo hayo Dkt. Nchimbi na Mhe. Balozi Vera wamejadiliana juu ya masuala mbalimbali yanayohusu namna ya kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Tanzania na Cuba na Chama Cha Mapinduzi na Chama Cha Kikomunisti cha Cuba (CPC).
Wakati wa mazungumzo hayo yaliyofanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam, leo Jumamosi Machi 5, 2024, Mhe. Balozi Vera ameishukuru Tanzania na CCM kwa jinsi ambavyo daima wamesimama na nchi hiyo katika nyakati zote.

Kupitia majadiliano hayo, pamoja na masuala mengine, viongozi hao wa pande zote mbili, wamejadiliana na kuainisha maeneo yatakayofanyiwa kazi kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha ushirikiano kati ya Wananchi wa Tanzania na Wananchi wa Cuba, Serikali za nchi zote mbili na vyama vinavyoongoza nchi hizo, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza mipango ya kubadilishana utaalam katika maeneo mbalimbali na kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kiuchumi.