Dkt.Kayandabila afunga Kongamano la 21 kwa Taasisi za Kifedha (COFI), TAMNOA waipa kongole BoT

NA GODFREY NNKO

NAIBU Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt.Dkt. Yamungu Kayandabila amefunga rasmi Kongamano la 21 kwa Taasisi za Kifedha (COFI) 2024 ambalo limefanyika kuanzia Machi 7 hadi 8, mwaka huu jijini Arusha.
Dkt.Kayandabila akizungumza kwa niaba ya Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba wakati akifunga kongamano hilo ambalo limewakutanisha zaidi ya wadau 1,000 kutoka ndani na nje ya nchi leo Machi 8, 2024 amesema, limekuwa kongamano la mfano.

Amesema,mada na mijadala iliyofanyika ambayo iliwakutanisha ana kwa ana washiriki wa kongamano hilo wakiwemo waliokuwa wanafuatilia kwa njia ya mtandao umewapa mikakati mbalimbali ya kuendelea kuimarisha ustahimilivu wa Sekta ya Fedha kwa nyakati zote.

Pia,ameishukuru Jumuiya ya Mabenki Tanzania (TBA) ambao wameshirikiana kwa pamoja na BoT kuhakikisha kongamano hilo linafanikiwa kwa viwango vya Kimataifa. 

Amesema, Serikali inatarajia kuona kwa vitendo matokeo ya waliyoyajadili, kukubaliana na kupendekeza yanafanyiwa kazi kwa ajili ya kuifanya Sekta ya Fedha nchini kuzidi kusonga mbele kwa ustawi bora wa Taifa na wananchi wake.
Katika kongamano hilo watoa mada mashuhuri kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Zimbabwe, Kenya, Marekani, Bangladesh na Nigeria wamewasilisha mawasilisho yao ambayo yalijikita zaidi kuhusu namna ya kuimarisha utahimilivu wa Sekta ya Fedha.

Aidha, wadau wote muhimu wa Sekta ya Fedha walipata fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu kuhusu mafanikio, changamoto na mikakati inayoweza kutekelezeka katika kuongeza ufanisi na tija ya kuleta maendeleo ya kifedha na kiuchumi nchini.

Miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika kongamano hilo la siku mbili ni ufanisi na uhimilivu wa taasisi za fedha wakati wa majanga.

Nyingine ni kuhusu uhimilivu wa sekta ya fedha katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi, jukumu la sheria mbalimbali, ubunifu na usimamizi wa vihatarishi.

Aidha, mada nyingine ilikuwa ni kuhusu ubunifu wa kiteknolojia katika utoaji wa huduma za kifedha,kichocheo cha ustahimilivu.

TAMNOA

Akizungumza katika hitimisho la kongamano hilo,Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni kwa niaba ya Umoja wa Kampuni za Simu Tanzania (TAMNOA) ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwaalika katika kongamano hilo muhimu nchini.
Mbeteni amesema kuwa, "Ninapenda kutoa shukurani zangu dhati kwa Benki ya Tanzania kwa kutupa mwaliko wa tukio hili muhimu, sisi ni wawakilishi kutoka taasisi za fedha zinazohusika na ukombozi wa kiuchumi kwa maslahi ya pamoja."

Pia, amesema umoja wao huo na wadau wote wa sekta ya fedha nchini wanaridhishwa na juhudi kubwa ambazo zinafanywa na BoT katika kusimamia malipo ya kielektroniki na mengineyo nchini ili kuwahakikishia usalama watoa huduma na wananchi kwa ujumla.

Mkurugenzi huyo ametoa pongezi hizo ikiwa licha ya hapa nchini fedha taslimu ndio njia maarufu ya kufanya malipo, pia kuna njia nyingine mbalimbali za kufanya malipo kama vile hundi, malipo ya kadi, malipo kwa njia ya mtandao, kwa njia ya simu na malipo ya kielektroniki.

Ikumbukwe kuwa, BoT ndiyo imekasimiwa mamlaka na Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya mwaka 2015 na Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 kusimamia na kudhibiti mifumo na huduma za malipo kwa watoa huduma za fedha yakiwemo mabenki na taasisi nyingine za fedha nchini.
Vile vile, BoT inashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Jumuiya ya Mabenki Tanzania, watoa huduma za miundombinu ya malipo kama TAMNOA, watumiaji huduma za malipo na wengineo katika kuboresha usalama na uendeshaji mzuri wa mifumo ya malipo nchini.

Wakati huo huo, Mbeteni ameipongeza BoT kwa kuja na Mfumo wa Taifa wa Malipo ya Papo kwa Papo (Tanzania Instant Payment System (TIPS) ambao umezinduliwa Machi 7, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Mpango.

Awali, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba alibainisha kuwa, kuzinduliwa kwa mfumo huo ni hatua muhimu katika kukidhi matarajio ya wananchi nchini.

"Benki Kuu ya Tanzania inaadhimisha hatua nyingine muhimu kwa kuzindua Mfumo wa Taifa wa Malipo ya Papo kwa Papo, yaani Tanzania Instant Payment System (TIPS).

"Uzinduzi wa mfumo huu unathibitisha dhamira ya Benki Kuu ya kukidhi matarajio ya wananchi katika kufanya miamala ya kifedha kwa haraka na kwa bei nafuu zaidi."

Gavana Tutuba alisema,mfumo huo umekuja wakati ambapo unahitajika sana ili kurahisisha zaidi shughuli za kifedha nchini na wanaamini kwamba utakidhi matarajio ya wananchi.

Alisema, mchakato wa kuanzisha mfumo wa TIPS ulifanywa na Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania,

Nyingine ni Mamlaka ya Mapato Tanzania, Ofisi ya Rais, na Mamlaka ya Serikali Mtandao pamoja na washirika wao wa maendeleo (Financial Sector Deepening Trust na Bill and Melinda Gates Foundation).

Alisema, majaribio ya mfumo yalianza mwezi Agosti 2022 na benki tatu na kampuni mbili za mawasiliano ya simu zilipata fursa ya kushiriki katika hatua za majaribio.

"Hadi tarehe 31 Januari 2024, benki 39 na kampuni 6 za mawasiliano ya simu zilikuwa zimeunganishwa. Kwa sasa, TIPS inawezesha miamala inayohusisha taasisi na mitandao mbalimbali (interoperable transfers) kwa matumizi kadhaa ikiwa ni pamoja na Mtu kwa Mtu (Person to Person - P2P).
"Mtu kwa Biashara (Person to Business - P2B), na Mtu kwa Wafanyabiashara (Person to Merchants - P2M) kwa kutumia teknolojia ya “QR code”. Mipango ya hivi karibuni ni kwa TIPS kuunganishwa na mfumo wa malipo ya Serikali wa GePG ili kurahisisha uhamishaji wa fedha na malipo ya Serikali."

Sambamba na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha (2023-2028) na Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21 - 2029/30, wenye lengo la kukuza huduma za kifedha za kidigitali ili kufikia uchumi usiotumia fedha taslimu, ni matarajio yetu kwamba matumizi ya TIPS yataongeza matumizi ya huduma za kifedha za kidigitali na kupunguza matumizi ya fedha taslimu nchini.

Gavana Tutuba alisema, Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kuhakikisha kuwa kuna utulivu wa bei na ustahimilivu katika sekta ya fedha kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki ya usimamizi na udhibiti.

Wakati huo huo, Mkurugenzi huyo wa Mpesa ameongeza kuwa, mfumo wa malipo ya fedha kwa njia ya simu una umuhimu mkubwa katika kukuza na kuimarisha utoaji wa huduma jumuishi za kifedha nchini.
"Kwa hiyo, uhusiano uliopo kati ya watoa huduma za kifedha kupitia simu za mikononi na sekta ya mabenki ni muhimu ili kufikisha huduma za kifedha kwa uwiano sawa katika nchi yetu kwa maana ya maeneo ya mijini na vijijini."

Kongamano hilo ambalo limeongozwa na kauli mbiu ya "Kuimarisha Ustahimilivu wa Sekta ya Fedha Nyakati za Changamoto za Kiuchumi" umeandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Mabenki Tanzania (TBA).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news