KILIMANJARO-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI kutuma timu ya watalaamu kufika Wilaya ya Mwanga na kuchunguza matumizi ya fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo.
Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kukagua ujenzi wa Hospitali hiyo akiwa ziarani mkoani Kilimanjaro.
Makamu wa Rais ameoneshwa kutoridhishwa na usimamizi wa ujenzi wa hospitali hiyo ikiwemo msimizi wa mradi huo ambaye ni mhandisi wa kilimo kutokuwa na vigezo vya kusimamia ujenzi wa hospitali.
Amesema miundombinu ya hospitali hiyo hairidhishi ikiwemo milango iliyo na viwango vya chini zaidi.
Amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kusimamia kikamilifu mradi huo na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.
Akizungumza na wananchi wa Mwanga, Makamu wa Rais amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuendelea kudumisha amani na utulivu katika eneo.
Amewasihi wananchi kuachana na tabia ya kulima dawa za kulevya aina ya mirungi na bangi katika maeneo ya milimani.
Amesema Wizara ya Kilimo kufanya utafiti na kubaini mazao yanayoweza kustawi katika kata zinazolima bangi na mirungi ili kupata mazao mbadala katika maeneo hayo yaweze kuwanufaisha wananchi.
Ameviagiza vyombo dola kuhakikisha vinaendeleza oparesheni ya kudhibiyti matumizi ya madawa ya kulevya katika eneo hilo.
Makamu wa Rais amesema Serikali itaongeza nguvu na uwezo wa Taasisi za uhifadhi (TAWA na TANAPA) kuendesha doria za kudhibiti wanyama wanaoharibu mali na mazao na hata kupoteza maisha ya watu.
Amesema tayari Serikali imeiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kuangalia upya namna ya kuongeza fidia kwa wahanga wa uharibifu wa makazi na mashamba.
Amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuongeza jitihada katika kupanda miti ili kuhifadhi mazingira.
Amesema, changamoto ya Ziwa Jipe (ambalo ndiyo chanzo cha maji cha Bwawa ya Nyumba ya Mungu) kujaa magugu maji inachangiwa na matumizi ya ardhi yasiyozingatia uhifadhi yanayosababisha mmomonyoko wa udongo ambao huingia ziwani humo.
Amewasihi wananchi kuzingatia maelekezo na ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kuhifadhi ardhi.