Dkt.Mpango azindua Mfumo wa Taifa wa Malipo ya Papo kwa Papo (TIPS)

NA GODFREY NNKO

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philp Mpango amezindua rasmi Mfumo wa Taifa wa Malipo ya Papo kwa Papo (Tanzania Instant Payment System (TIPS).
Dkt.Mpango amezindua mfumo huo muda mfupi baada ya kufungua Mkutano wa 21 kwa Taasisi za Fedha (COFI) katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.

Mkutano huo ambao unaongozwa na kauli mbiu ya "Kuimarisha Ustahimilivu wa Sekta ya Fedha Nyakati za Changamoto za Kiuchumi" umeandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Mabenki Tanzania (TBA).

"Kwa kuzingatia kasi ya mabadiliko na maendeleo ya teknolojia duniani, tunashuhudia ongezeko kubwa la matumizi ya malipo kwa njia za kidigitali, hasa katika sekta za benki, biashara ya bima, mifuko ya hifadhi ya jamii na huduma nyingine."
Dkt.Mpango amesema, mabadiliko hayo yanapelekea uhitaji wa kuhama kutoka kwenye matumizi ya pesa taslimu kwenda kwenye njia za malipo za kielektroniki ili kupunguza hatari zinazohusiana na kutumia pesa taslimu na kuongeza urahisi wa ufanyaji malipo.

"Hivyo basi, natoa wito kwa watoa huduma wa mifumo ya malipo kuendelea na ubunifu ambao utawezesha na kudumisha utengenezaji wa bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji mbalimbali ya jamii yetu kuendana na mahitaji ya jamii yanavyobadilika.

"Kwa muktadha huu, napenda kutambua mafanikio ya kuundwa kwa Mfumo wa Taifa wa Malipo ya Papo kwa Papo yaani Tanzania Instant Payment System (TIPS).

"Ninatarajia kwamba mfumo wa TIPS, kama ilivyoelezwa na Gavana wa Benki Kuu, utasaidia kuendeleza huduma rasmi za kifedha na kupunguza gharama za miamala. Napenda kuipongeza Benki Kuu ya Tanzania na taasisi zote zilizoshiriki katika kuunda mfumo huu wa malipo."
Vile vile, Makamu wa Rais Dkt.Mpango amempongeza Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania kwa kuanza kutumia mfumo mpya wa utekelezaji wa sera ya fedha unaotumia riba.

Amesema, hiyo ni mojawapo ya hatua muhimu zilizofikiwa hivi karibuni katika sekta ya fedha. "Ni matarajio yangu kuwa mfumo huu mpya utaimarisha ufanisi wa sera ya fedha katika mazingira ya sasa ya kiuchumi na hivyo kutoa ishara kwa riba za mikopo inazotolewa na taasisi za fedha ili kuchochea uwekezaji na ukuaji wa uchumi."

Awali,Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amebainisha kuwa, kuzinduliwa kwa mfumo huo ni hatua muhimu katika kukidhi matarajio ya wananchi nchini.

"Leo, Benki Kuu ya Tanzania inaadhimisha hatua nyingine muhimu kwa kuzindua Mfumo wa Taifa wa Malipo ya Papo kwa Papo, yaani Tanzania Instant Payment System (TIPS).
"Uzinduzi wa mfumo huu unathibitisha dhamira ya Benki Kuu ya kukidhi matarajio ya wananchi katika kufanya miamala ya kifedha kwa haraka na kwa bei nafuu zaidi."

Gavana Tutuba amesema,mfumo huo umekuja wakati ambapo unahitajika sana ili kurahisisha zaidi shughuli za kifedha nchini na wanaamini kwamba utakidhi matarajio ya wananchi.

Amesema, mchakato wa kuanzisha mfumo wa TIPS ulifanywa na Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania,

Nyingine ni Mamlaka ya Mapato Tanzania, Ofisi ya Rais, na Mamlaka ya Serikali Mtandao pamoja na washirika wao wa maendeleo (Financial Sector Deepening Trust na Bill and Melinda Gates Foundation).
Amesema, majaribio ya mfumo yalianza mwezi Agosti 2022 na benki tatu na kampuni mbili za mawasiliano ya simu zilipata fursa ya kushiriki katika hatua za majaribio.

"Hadi tarehe 31 Januari 2024, benki 39 na kampuni 6 za mawasiliano ya simu zilikuwa zimeunganishwa.

"Kwa sasa, TIPS inawezesha miamala inayohusisha taasisi na mitandao mbalimbali (interoperable transfers) kwa matumizi kadhaa ikiwa ni pamoja na Mtu kwa Mtu (Person to Person - P2P).

"Mtu kwa Biashara (Person to Business - P2B), na Mtu kwa Wafanyabiashara (Person to Merchants - P2M) kwa kutumia teknolojia ya “QR code”. Mipango ya hivi karibuni ni kwa TIPS kuunganishwa na mfumo wa malipo ya Serikali wa GePG ili kurahisisha uhamishaji wa fedha na malipo ya Serikali."

Sambamba na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha (2023-2028) na Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21 - 2029/30, wenye lengo la kukuza huduma za kifedha za kidigitali ili kufikia uchumi usiotumia fedha taslimu, ni matarajio yetu kwamba matumizi ya TIPS yataongeza matumizi ya huduma za kifedha za kidigitali na kupunguza matumizi ya fedha taslimu nchini.
Gavana Tutuba amesema, Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kuhakikisha kuwa kuna utulivu wa bei na ustahimilivu katika sekta ya fedha kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki ya usimamizi na udhibiti.

"Benki Kuu pia itaendelea kuhakikisha kuwa sekta ya fedha inaendelea kubeba jukumu kubwa katika kukuza uchumi.

"Nichukue fursa hii tena kuzishukuru Serikali zetu zote mbili yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuweka mazingira mazuri kwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja na sekta ya fedha.
"Pia, nawapongeza Jumuiya ya Mabenki Tanzania (TBA), pamoja na Taasisi ya Kuongeza Ustawi wa Sekta ya Fedha (FSDT) kwa kushirikiana nasi kuandaa kongamano hili,"amebainisha Gavana Tutuba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news