MSAJILI wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi Tanzania (CRB), Mhandisi Rhoben Nkori amewakemea baadhi ya Makandarasi wanaofanya kazi kwa mazoea kuacha tabia hiyo huku akieleza Bodi haitasita kuwafutia usajili wa kampuni zao.
Alisema kwa sasa Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa miradi mingi kutekelezwa na Makandarasi wazawa lakini kuna baadhi wamekuwa wakitumia fursa hiyo kuijengea taswira mbaya tasnia hiyo kwa kufanya kazi bila kuzingatia weledi.
Hayo aliyasema Machi 8,2024 jijini Dar es Salaam wakati akiongea na Makandarasi zaidi ya 170 waliokuwa wakishiriki mafunzo ya siku tatu yaliyokuwa yanalenga kuwajengea uwezo na ujuzi wa namna ya kuandaa zabuni, kujaza mikataba, utekelezaji wa mikataba ya ujenzi, elimu ya kodi na namna ya kuzisimamia na kuboresha kazi zao.