ARUSHA-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ikiongozana na Waziri wa Madini,Mhe. Anthony Mavunde leo imetembelea Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kinachotoa Mafunzo ya Uongezaji Thamani Madini kwa ajili ya kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la kituo hicho ambalo litakuwa mahsusi kwa utoaji wa mafunzo ya kuongeza thamani,minada ya madini ya vito na maonesho ya madini.
Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,Dkt. David Mathayo amepongeza serikali kwa jitihada za kuboresha mafunzo katika eneo la uongezaji thamani madini ya vito na kutoa maagizo ya uharakishwaji wa taratibu za kuanza ujenzi wa mradi mapema ili manufaa yake kwa watanzania yaonekane
Akizungumza katika Ziara hiyo Waziri wa Madini,Mhe. Anthony Mavunde amesema kwamba jengo hilo pacha (twin tower) lenye thamani ya shilingi Bilioni 35 litakuwa na miundombinu mbalimbali ikiwemo madarasa, karakana (viwanda) vya uongezaji thamani madini, maabara za madini ya vito na bidhaa za usonara, mineral gallery, ofisi, mabweni ya wanafunzi, kantini na maduka.
Mheshimiwa Mavunde aliongeza pia kwamba Jengo hilo litafungamanisha mafunzo ya uongezaji thamani madini pamoja na viwanda vya uchakataji na biashara ya madini nchini kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo ili kuimarisha umahiri. Mradi huu pia, uhahusisha utolewaji wa mafunzo kwa watumishi kwa lengo la kuwaongezea uwezo (capacity building) pamoja na ununuzi wa vitendea kazi.
Akitoa taarifa ya Mradi huo Kaimu Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC),Mhandisi Ally Maganga ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa ya sekta ya madini na hasa kupitia uongezaji thamani wa madini ya vito ambao utekelezaji wake utachangiwa na kukamilika kwa mradi huu mkubwa na kutumia fursa hiyo pia kuiahidi kamati ya Bunge juu ya usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa mradi huu kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.