DAR ES SALAAM-Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umesema kuwa Kitita cha huduma kwa wanachama wake kimeboreshwa na sasa kinajumuisha huduma mbalimbali zikiwemo huduma za kibingwa na bobezi.
Maboresho haya yanatokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika miundombinu na wataalamu katika Sekta ya afya.
Haya yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga wakati akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam wiki hii.
“Mathalani ukiangalia gharama za Saratani zilizolipwa na Mfuko mwaka 2022/23 zilikuwa ni Shilingi bilioni 32.46 ukilinganisha na Shilingi bilioni 12.25 mwaka 2021/22, gharama za matibabu ya Figo zilikuwa Shilingi bilioni 35.40 na mwaka 2021/2022 ilikuwa Shilingi bilioni 11.45 hivyo unaweza kuona ni namna gani Mfuko umehakikisha unajumuisha huduma hizi,” alisema Bw. Konga.
Akizungumzia uboreshaji wa huduma kwa wanachama, alisema Mfuko umeimarisha utambuzi wa wanufaika vituoni kwa kutumia alama za vidole na sura ili kurahisisha utambuzi wa wanachama wakati wa kupata huduma za matibabu.
“Kwa sasa mfumo wetu wa TEHAMA unamuwezesha mwanachama kujisajili, kupata namba ya malipo kwa kutumia mfumo wa kielektroniki, matumizi ya namba za utaifa kwa baadhi ya makundi ya wanachama ikiwa ni mbadala wa vitambulisho na kuimarisha utambuzi lakini pia kuwepo kwa mfumo unaoshughulikia malalamiko na kupokea maoni ya wadau wa Mfuko,” alisema Bw. Konga.
Alisema kuwa,katika kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Mfuko umefanikisha kusogeza huduma karibu na wanachama kwa kuongeza ofisi ndogo za NHIF (Ubungo, Kigamboni na Gongolamboto) ili kuwezesha kuwafikia wananchi kiurahisi zaidi.
Alisema kuwa,lengo la kufanyika kwa maboresho ni kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa kuzingatia mahitaji halisi ya tiba kwa sasa hivyo akatumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kujiunga na NHIF ili waweze kuwa na uhakika wa huduma za Matibabu.