NA GODFREY NNKO
SERIKALI imesema, katika kipindi cha kuanzia Machi 2021 hadi Februari 2024 Wizara ya Madini imefanikiwa kuiendeleza sekta kwa namna mbalimbali ikiwemo kukusanya maduhuli yatokanayo na ada mbalimbali, mirabaha, faini na penati na kufikisha kiasi cha shilingi trilioni 1.93.
Hayo yamesemwa leo Machi 24, 2024 jijini Dar es Salaam na Msemaji Mkuu wa Serikali,Mobhare Matinyi wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarani.
Amesema,mwaka 2021/22 sekta hiyo ilikuwa shilingi bilioni 591.5 lakini hadi kufikia mwaka 2023/24 imefikia shilingi bilioni 690.4.
“Aidha, katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022 mauzo ya madini mbalimbali yalikuwa shilingi bilioni 157.34 lakini kufikia kipindi cha Machi 2023 hadi Februari 2024 mauzo yamefikia shilingi bilioni 476.8,” amesema Matinyi.
Kwa upande wa Sekta ya Kilimo, Matinyi amesema kuwa, bajeti imeongezeka kutoka shilingi bilioni 294.16 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni shilingi bilioni 970.78 mwaka wa fedha 2023/2024.
Pia, matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 320,233 kwa mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia tani 580,628 kwa mwaka wa fedha 2022/23.
“Bajeti ya maendeleo ya umwagiliaji imeongezeka kutoka shilingi bilioni 46.5 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 361.5 mwaka 2023/24 ambapo wataalam wa kilimo 320 wameajiriwa na kusambazwa katika ofisi za umwagiliaji zilizopo katika wilaya 139.
"Na mitambo 15 na magari 53 vimenunuliwa kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji."
Amesema,eneo la umwagiliaji limeongezeka kutoka hekta 694,715 mwaka 2020/2021 hadi hekta 727,280.6 mwaka 2022/2023.
Pia, ameema Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa skimu za umwagiliaji zenye hekta 95,000 zilizoanza mwaka 2022/2023 pamoja na kuanza skimu mpya zenye ukubwa hekta 95,000 kwa mwaka 2023/2024, ambapo kukamilika kwake kutaongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 917,280.
“Programu ya Vijana ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Build Better Tomorrow-BBT). Mradi unashirikisha vijana 688, ambao wameanza kilimo biashara katika shamba la Chinangali II,” amesema Matinyi.
Kuhusu Sekta ya Ufugaji na Uvuvi,Matinyi amesema katika kipindi cha miaka mitatu 2021/22 hadi mwaka 2023/24, bajeti ya sekta ya mifugo imekua ikiongezeka kwa kasi.
Amesema, bajeti hiyo imeongezeka kutoka shilingi 47,844,950,000/- mwaka 2021/22 hadi shilingi 112,046,777,000/- mwaka 2023/24.
Katika kipindi cha miaka mitatu, 2021/22 hadi mwaka 2023/24 amesema, bajeti ya sekta ya uvuvi imepanda kutoka shilingi 121,350,046,999/- mwaka 2021/22 hadi shilingi 183,874,156,000 mwaka 2023/24.
“Ili kuhakikisha Serikali inarasimisha shughuli za uvuvi, kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Januari 30, 2024, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua zoezi la ugawaji wa boti 160 na vizimba 222, kwa ajili ya makampuni, watu binafsi na vikundi vya wavuvi kupata vitendea kazi hivyo kwa njia ya mkopo usio na riba. Sasa bandari ya uvuvi inajengwa Kilwa Masoko,” amesema Matinyi