Mahakama yafuta shauri la kimaadili alilofungua Wakili Madeleka

NA SETH KAZIMOTO
MAHAKAMA KUU

HIVI karibuni, Wakili Peter Madeleka alibisha hodi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha kuomba kibali cha kufungua shauri dhidi ya Kamati ya Maadili ya Mawakili baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasilisha maombi ya shauri la nidhamu mbele yake.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga aliyesikiliza shauri lililofunguliwa na Wakili Peter Madeleka, ambaye amesshindwa kuliendesha.

Wakili huyo alifungua maombi hayo tarehe 26 Februari, 2024 kwa lengo la kuizuia Kamati hiyo kumuita mbele yake.

Shauri hilo lilipangwa mbele ya Jaji Joachim Tiganga na Mahakama ikampangia awapelekee wito upande wa pili ambao ni Wakili Mkuu wa Serikali kwa nia ya kujibu maombi hayo.

Maombi hayo yakapangwa kusikilizwa siku ya tarehe 3 Machi, 2024 ambapo Wakili Madeleka alipofika mahakamani, alileta pingamizi dhidi ya Wakili wa Serikali aliyeandaa kiapo, kwamba hakuwa kwenye orodha ya Mawakili wa Serikali.

Pingamizi hilo lilisikilizwa na kuamuliwa tarehe 12 Machi, 2024 ambapo Mahakama ilisema Wakili huyo alikuwa kwenye orodha ya Mawakili wa Serikali, hivyo alikuwa na uwezo wa kuandaa kiapo hicho.

Kufuatia uamuzi huo, Mahakama ilipanga kusikiliza maombi yake ya msingi tarehe 15 Machi, 2024.

Shauri lilipoitwa siku hiyo kwa ajili ya kusikilizwa, Wakili Madeleka aliibua tena pingamizi jingine kwamba Wakili wa Serikali, Edwin Webiro hajatangazwa kwenye Gazeti la Serikali.

Hoja hiyo ilisikilizwa na kutolewa uamuzi tarehe 25 Machi, 2024 ambapo Mahakama ilikataa pingamizi hilo na ikamtaka Wakili Madeleka aendelee na maombi yake ya msingi aliyoleta mahakamani.

Baada ya Mahakama kumtaka Wakili Madeleka alete hoja zake kwenye maombi ya msingi, yeye alisema kuwa ameshafungua shauri la rufaa katika Mahakama ya Rufaa, hivyo hayuko tayari kusikilizwa.

Hivyo, Mahakama ilimtaka atoe uthibitisho kama tayari ameweka nia ya kukata rufaa (Notice of Appeal).

Wakili Madeleka aliiambia Mahakama kwamba aliwasilisha nia hiyo kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Kusajili Mashauri Mahakamani (e-CMS) na akaomba Mahakama iangalie kwenye mfumo huo.

Mahakama iliangalia na kubaini kuwa nia hiyo ya kukata rufaa haikuwa imewasilishwa katika mfumo aliotaja mleta maombi.

Hivyo, Mahakama ilimweleza mleta maombi kuwa hapakuwa na sababu za msingi za kuizuia Mahakama kusikiliza shauri hilo.

Pamoja na kupewa maelezo hayo, Wakili Madeleka aliendelea kusisitiza kuwa yeye hayuko tayari kusikilizwa kwa sababu amekata rufaa na alimtaka Jaji Joachim Tiganga ajiondoe kusikiliza shauri hilo kwa sababu hana imani naye.

Baada ya kupitia na kupima hoja za mleta maombi za kukataa kuendelea na shauri hilo, Jaji Tiganga alikataa kujiondoa na kumtaka mleta maombi alete hoja zake katika shauri la msingi ili asikilizwe na hatimae kutolewa maamuzi.

Hata hivyo, Wakili Madeleka aligomea maelekezo hayo, akasimama na kuondoka mahakamani.

Kufuatia tabia hiyo ya utovu wa nidhamu aliyoinesha Wakili Madeleka, Jaji Tiganga aliuliza upande wa wajibu maombi kama walikuwa na hoja yoyote.

Wajibu maombi wakaomba maombi hayo yafutwe kwa kuwa Wakili Madeleka ameshindwa kuyaendesha licha ya Mahakama kumpa nafasi hiyo mara kwa mara.

Mahakama iliridhia na ikaamua kufuta maombi hayo baada ya mletaji, yaani Wakili Madeleka mwenyewe kukataa kuyaendesha na kuondoka mahakamani wakati shauri hilo lilikuwa limeiva kwa ajili ya kusikilizwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news