Mamia waendelea kuhama Ngorongoro kwa hiyari yao

ARUSHA-Katika hali inayoonesha kuwa wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro wamepuuza ushawishi wa baadhi ya watu wanaotaka wasiondoke katika eneo hilo, leo tarehe 3 Machi, 2024 jumla ya kaya 76 zenye watu 451 na mifugo 1,259 wameamua kuondoka kwa hiyari.

Ni ndani ya hifadhi kuelekea katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga na Kijiji cha Makao wilayani Meatu mkoani Simiyu.
Katika hafla ya kuwaaga wananchi hao iliyofanyika makao makuu ya zamani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro baadhi ya wananchi wamesema kuwa, wameamua kuondoka ndani ya hifadhi kutokana na kufanya mawasiliano na wenzao waliokwishahamia katika Kijiji cha Msomera na kupata taarifa kuwa maisha katika Kijiji hicho ni bora kulinganisha na kuishi hifadhini.
“Hatuondoki kwa kukurupuka,tunafanya mawasiliano na wenzetu ambao tayari wameshakwenda Msomera na wakati mwingine tumekuwa tukifika katika Kijiji hicho kufanya uchunguzi, binafsi kabla ya maamuzi haya nilikwenda Msomera kufanya uchunguzi wangu na kushuhudia maendeleo makubwa katika kijiji hicho, ndiyo maana niliporudi Ngorongoro niliishawishi familia yangu na leo tumeamua kuondoka;alisema bwana Mathayo Laizer mmoja wa wakazi walioamua kuhama kwa hiyari.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Richard Kiiza amewaambia wananchi hao kuwa serikali imejipanga vizuri kuhakikisha wananchi hao wanapata haki zao zote za msingi ikiwa ni pamoja na huko wanakokwenda kuwepo kwa miundo mbinu mizuri itakayowawezesha kuboresha maisha yao ya kila siku.
Kamishna Kiiza amesema kila mwananchi ambaye yupo tayari kuhama atasafirishwa kwa wakati na kupata stahiki zake zote bila urasimu huku akisisitiza kuwa zoezi la uandikishaji wa wananchi wanaotaka kuhama kwa hiyari linaendelea kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya Tarafa ya Ngorongoro.

Katika taarifa yake Kaimu Meneja Mradi wa zoezi hilo Afisa Uhifadhi Mkuu Flora Assey amesema zoezi la kuhamasisha na kuandikisha wananachi kuhama kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro linaendelea kwa kasi kutokana na wananchi kupata uelewa mpana wa jinsi wanavyoweza kupata fursa za kujiendeleza kiuchumi katika maeneo wanayoelekea.
Mwakilishi kutoka wizara ya Maliasili na Utalii Bw.John Mapepele aliwapongeza wananchi hao kutokana na kuamua kuondoka ndani ya hifadhi na kusisitiza kuwa wizara itaendelea kusimamia zoezi hilo kwa karibu ili kuhakikisha kila mtu anayetaka kuondoka anapewa fursa hiyo na misingi ya sheria, taratibu na haki za binadamu itazingatiwa.
Serikali inaendelea na zoezi la kuhamisha watu kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro lengo likiwa ni kuboresha maisha ya wananchi hao nje ya hifadhi hasa ikizingatiwa kwamba katika eneo hilo wananchi hao wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo uwepo wa fursa chache za kujiendeleza kiuchumi na kijamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news