NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imevunja rekodi ya kipekee baada ya miezi mitatu kukusanya shilingi bilioni 6.14 licha ya kukasimiwa kukusanya shilingi bilioni 6.45 kwa mwaka.
Hayo yamesemwa leo Machi 13, 2024 jijini Dar es Salaam na Prof. Joseph Ndunguru ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo katika kikao kazi na wahariri, waandishi wa vyombo vya habari nchini kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
"Katika mwaka wa fedha 2023/2024 mamlaka ilikasimia kukusanya kiasi cha fedha cha shilingi bilioni 6,454,437,453, mapato ya ndani na katika kipindi cha miezi mitatu tu kwa maana ya Julai 2023 hadi Septemba 2023.
"Mamlaka imeweza kukusanya kiasi cha shilingi 6,143,965 337.61 sawa na asilimia (95.2 ya makadirio ya makusanyo ya mwaka mzima kutoka kwenye vyanzo vyake mbalimbali vya mapato ya ndani."
Prof.Ndunguru amesema, hiyo inadhirisha kwamba hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha, mamlaka hiyo itaweza kukusanya zaidi ya asilimia 100 ya makadirio hayo.
Hivyo, kuweza kuongeza kiasi cha gawio lake kwa Serikali Kuu asilimia 15 kutoka shilingi 968,165,000.62 walizotarajia hadi shilingi 3,686,379,202.56 kwa mwaka.
Vile vile, amebainisha kuwa, kwa kipindi cha mwezi Oktoba mpaka Desemba 2023 mamlaka hiyo imekusanya shilingi 5, 352, 196, 967.04 ikiwa ni madhuhuli ya Serikali.
“Na kwa kipindi cha Januari mpaka Machi 6, 2024 mamlaka imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.7.”
Amesema mafaniko hayo yanapatikana ikiwa, mamlaka hiyo imeanza kazi rasmi Julai, 2022 huku ikiundwa kwa Sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Na.4 ya mwaka 2020 (Plant Health Act No. 04 of 2020".
Ni kwa kuunganisha iliyokuwa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu ya Ukanda wa Kitropiki ( TPRI)-Sheria Na.18 ya 1979) na Kitengo cha Afya ya Mimea kilichokuwa chini ya Wizara ya Kilimo (PHS)-Sheria Na.13 ya mwaka 1997).
Amesema, mamlaka hiyo iliundwa ili kuweka mfumo wa pamoja wa kisheria wa usimamizi na udhibiti wa afya ya mimea, mazao ya mimea na viuatilifu.
Lengo likiwa ni kukidhi matakwa ya masoko na mikataba ya Kimataifa na kuweka mazingira salama kwa afya ya binadamu, wanyama na mimea kwa kuwa na matumizi sahihi na salama ya viuatilifu nchini.
Hata hivyo, licha ya mamlaka hiyo kuwa chini ya Wizara ya Kilimo pia ni miongoni mwa taasisi na mashirika ya umma ambayo yanasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
TR ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.
Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa ofisi inayojitegemea kimuundo.
Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) ofisi ilikabidhiwa majukumu ya shirika hilo.
Kikao kazi cha leo na TPHPA ni mwendelezo wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kuzikutanisha taasisi na mashirika hayo ya umma na wahariri ili ziweze kuelezea walikotoka, walipo na wanapoelekea.
Dhamira ikiwa ni ili umma ambao ndiyo wamiliki wa taasisi hizo waweze kupata mwelekeo wake na kufahamu mafanikio yao.
PHBIU
Mbali na hayo, Prof.Ndunguru amebainisha kuwa, mamlaka hiyo imeanzisha Kituo cha Kisasa cha Kuchakata Taarifa za Mazao, Masoko na Visumbufu (Plant Health and Biosafety Intelligence Unit).
Amesema, kituo hicho kipo makao makuu ya mamlaka hiyo jijini Arusha ambapo kinawezesha kufungua masoko na kuyaendeleza nchini.
Prof. Ndunguru amefafanua kuwa,kituo pia kitapokea na kuchakata taarifa kutoka kanda zake saba ikiwemo Kanda ya Mashariki ambayo inaundwa na mikoa ya Dar-es-salaam, Tanga, Pwani na Morogoro na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo inaundwa na mikoa ya Mbeya, Songwe, lringa na Njombe.
Nyingine ni Kanda ya Kusini ambayo inaundwa na mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma ikiwemo Kanda ya Ziwa ambayo inaundwa na mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara na Kagera.
Vile vile kuna Kanda ya Kati ambayo inaundwa na mikoa ya Dodoma and Singida ikiwemo ya Magharibi ambayo inaundwa na mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa na Tabora.
Kanda nyingine ni ya Kaskazini ambayo inaundwa na mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara. “Hivyo, tumedhamiria kuwa chombo mahiri kinachoongoza katika kutoa huduma za afya ya mimea katika udhibiti wa visumbufu vya mimea na viuatilifu kwa kiwango cha Kimataifa.”
Amesema, majukumu ya kituo ni pamoja na uchakataji wa takwimu za mazao na visumbufu zilizopo katika portal kama ATMIS na kutengeneza taarifa kwa ajili ya maamuzi.
“Lakini pia utambuaji na ubainishaji wa visumbufu kwa kutumia teknolojia ya remote sensing na GIS.” Pia, amesema mamlaka inatekeleza kwa vitendo Agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Msajili wa Hazina la kufanya mageuzi katika Taasisi zake za Serikali ( Reform, Rebuild, Resilience and Reconciliation (4Rs) ili kuleta tija.
Amesema, kituo hicho ni sehemu ya utekelezazji wa majukumu ya mamlaka ambayo ni kuwezesha masoko ya mimea na mazao ya mimea hapa nchini na Kimataifa kwa kufanya ufuatiliaji wa visumbufu na uchambuzi wa hatari ya visumbufu.
Jukumu lingine amesema ni kudhibiti uagizaji, usafirishaji, utengenezaji, usambazaji, uuzaji, na matumizi ya viuatilifu na vifaa vya unyunyiziaji wa viuatilifu ili kuleta tija katika Kilimo.
“Na kulinda afya ya binadamu na mazingira kwa usimamizi bora na endelevu wa viuatilifu na afya ya mimea ikiwemo kutoa huduma ya utambuzi na uhifadhi wa bioanuai za mimea na vinasaba vya mazao,”
Jukumu lingine, Prof.Ndunguru amesema ni kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa usafi wa mimea na mazao mashambani, ghalani na mipakani ili kuzuia kuenea kwa visumbufu.
Mbali na hayo akizungumzia umuhimu wa sekta ya kilimo katika uchumi wa nchi amesema kuwa, asilimia kubwa ya malighafi inayotegemewa viwandani inatoka katika sekta ya kilimo
Aidha, ili kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo,Prof.Ndunguru ametaja mambo sita muhimu ya kuzingatia ambayo ni pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi.
Pia kuwekeza kwenye utafiti, jambo ambalo serikali imefanya kwa kiasi kikubwa kwani.bajeti ya kilimo imefikia shilingi bilioni 970.78 na nguvu kubwa imeelekezwa kwenye utafiti wa mbegu bora.
“Ikiwemo uzalishaji wa mbegu na miche bora, usambazaji wa mbegu na miche ya ruzuku, kuwekezaji kwenye huduma za ugani na ujenzi wa miundombinu ya kilimo, vyote hivi ni kufanya kilimo kinachotumia sayansi na teknolojia na hivi vinaenda kuleta faida kubwa katika kilimo.
“Kwa hiyo,katika utekelezaji wa majukumu yake, mamlaka inafanya kazi kupitia ofisi yake yenye makao makuu jijini Arusha, pamoja na kanda zake saba zilizogawanyika pote Tanzania Bara, na vituo rasmi vya ukaguzi 36 vinavyojumuisha mipaka ya nchi kavu, bandari na viwanja vya ndege."
Utambuzi
Wakati huo huo, Prof.Ndunguru amesema, mamlaka hiyo imefanikiwa kukusanya, kutambua na kuhifadhi sampuli kavu 1,643 za mimea kwa matumizi ya rejea za utafiti.
“Hata hivyo, mamlaka inaendelea kuhifadhi jumla ya sampuli kavu za mimea zipatazo 300,000.”
Pia, amesema mamlaka imeweza kukusanya jumla ya sampuli hai 764 za nasaba za mimea ya aina mbalimbali na kuhifadhi katika benki ya mbegu.
Prof.Ndunguru amebainisha kuwa, mamlaka inaendelea kuhifadhi jumla ya sampuli 12,000 za nasaba za mimea.
“Na mamlaka imeweza kudhibiti baa la panya katika eneo la ekari 285,195.15 zilizokuwa na mazao mbalimbali, na jumla ya wakulima 201,549 walihudumiwa katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Pwani, Lindi, Mtwara Manyara na Arusha
“Hivyo, mafunzo ya namna ya kuwatambua aina ya panya na mbinu za kudhibiti yalitolewa.”