DAR ES SALAAM-Serikali ya Tanzania na Serikali ya Italia zimekutana na kuainisha sekta za kipaumbele zitakazonufaika na mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan).
Sekta zinazotarajiwa kunufaika na Mpango wa Mattei ni Kilimo, Nishati, Elimu, Afya na Uchumi wa Buluu.
Akizungumza wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo (Mb,) amesema mkutano huo umelenga kujadili utekelezaji wa mpango mpya wa kimkakati wa Mattei kati ya Tanzania na Italia.
Prof. Mkumbo amesema katika mpango huo vipaumbele vikubwa vimetolewa katika sekta za elimu, kilimo, maji na nishati na kuongeza kuwa maeneo waliyobainisha yanaendena na vipaumbele vya Serikali ya Tanzania ambavyo ni elimu, afya, nishati, miundombinu na kilimo.
“Tumekubalina kuanza kutengeneza miradi kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu. Miradi hiyo inatekelezwa katika nchi nne za Afrika ambazo ni Tanzania, Ethiopia, Kenya na Uganda. Tumekubaliana kujikita katika maendeleo ya zao la kahawa,” amesema Prof. Mkumbo.
Prof. Mkumbo ameongeza kuwa Tanzania imekuwa ikipambana kuongeza uzalishaji wa mazao hususan kahawa, kuongeza masoko hasa katika bara la Ulaya pamoja na kuongeza thamani katika mazao.
“Hivyo kupitia Mpango wa Mattei Tanzania itasafirisha mazao yenye thamani nje ya nchi na kuliwezesha Taifa kupata fedha za kigeni,” amesema Waziri Mkumbo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia, Mhe. Stefano Gatti amesema Mpango wa Mattei umetoa kipaumbele kwa Tanzania katika sekta ya Kilimo hususan zao la kahawa ambapo nchi hizo mbili zitaendelea kushirikiana kuendeleza zao la Kahawa.
"Sisi kama Serikali tutashirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha zao la Kahawa kutoka Tanzania tunaliongezea thamani pamoja na kuwanufaisha wakulima wa zao hilo licha ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Mhe. Gatti.
Mhe. Gatti aliongeza kuwa Mpango wa Mattei utaihusisha sekta ya uchumi wa buluu – Zanzibar pamoja na kutoa elimu katika sekta zitakazo nufaika na Mpango wa Mattei.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Italia katika kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya pande zote mbili.
Mpango wa Mattei umelenga kuimarisha malengo ya maendeleo endelevu yenye lengo la kuboresha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Italia.
“Kupitia Mpango wa Matei, Italia na bara la Afrika sasa wamekuja na dhana mpya ya ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ambayo yatakuza kiuchumi kwa viwango vya juu zaidi,” alisema Balozi Mussa.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na usshirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Marco Lombardi, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na maafisa mbalimbali waandamizi wa serikali kutoka wizara za kisekta.
Mwezi Januari 2024, Tanzania ilichaguliwa kuwa moja ya nchi za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan) ambapo kiasi cha Euro bilioni 5 za awali kilitengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Miradi hiyo ya kipaumbele kupitia Mpango mpya wa Kimkakati wa Mattei (Mattei plan) ipo katika sekta ya nishati, elimu na kilimo.