Mkutano wa 21 wa Taasisi za Fedha (COFI) wakutanisha wadau 1,000 Arusha

NA GODFREY NNKO

ZAIDI ya washiriki 1,000 wamejumuika pamoja katika Mkutano wa 21 wa Taasisi za Fedha (COFI) unaoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Mkutano huo ambao unaongozwa na kauli mbiu ya "Kuimarisha Ustahimilivu wa Sekta ya Fedha Nyakati za Changamoto za Kiuchumi" umeandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Mabenki Tanzania (TBA).

Hayo yamesema leo Machi 7, 2024 na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Emmanuel Tutuba katika hafla ya ufunguzi ambapo kongamano hilo limefunguliwa na mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Mpango.

"Kongamano hili la siku mbili linawakutanisha washiri zaidi ya 1,000 ambapo washiriki 43 wamethibitisha kushiriki kwa njia ya mtandao.

"Kwa hiyo ni mkutano ambao tunaita ni high breed, kongamano hili huwa linafanyika kila baada ya miaka miwili.

"Kongamano hili, linatoa fursa kwa wadau wote muhimu wa Sekta ya Fedha kupata fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu kuhusu mafanikio, changamoto na mikakati inayoweza kutekelezeka katika kuongeza ufanisi na tija ya kuleta maendeleo ya kifedha na kiuchumi nchini.

"Kama tulivyofanya kongamano la 20 jijini Dodoma,katika mwaka wa fedha 2021/22 Sekta ya Fedha imeendelea kutekeleza maboresho mbalimbali ya kimfumo, kimuundo na kiutawala hali iliyowezesha sekta hii kuongeza mchango wake na pia, kuongeza kasi katika ukujai wa uchumi kwa mwaka 2023."

Gavana Tutuba amesema,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imetoa umuhimu mkubwa katika kusimamia maendeleo ya Sekta ya Fedha nchini.

Pia,amezishukuru wizara na wadau wote kwa namna ambavyo wamekuwa wakiwapa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yao ili kuhakikisha Sekta ya Fedha inaendelea kuwa na matokeo chanya kwa ustawi bora wa uchumi na maendeleo ya nchi.

Gavana Tutuba amesema,uwezo wa taasisi za fedha na utayari wa kukabiliana na changamoto wakati wote ni muhimu sio tu kwa utulivu na ustahimilivu wa uchumi, bali pia ni kwa ajili ya kudumisha ustawi wa jamii na siasa.

"Kama alivyosema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki, kaulimbiu ya Kongamano hili la 21 ni "Kuimarisha Ustahimilivu wa Sekta ya Fedha Nyakati za Changamoto za Kiuchumi".

"Chaguo la kaulimbiu hii limechochewa na athari za changamoto zinazotokana na janga la UVIKO-19, migogoro ya kikanda ya kisiasa kwa baadhi ya nchi duniani, na changamoto za tabianchi ambazo zimesababisha pamoja na mambo mengine, kuwepo kwa athari hasi katika mnyororo wa usambazaji bidhaa duniani, ongezeko la bei za bidhaa, na hali ngumu ya kifedha duniani.

"Katika mazingira kama haya, ni muhimu hapa Tanzania na katika ukanda wetu kuwa na sekta ya fedha iliyo imara na madhubuti unajidhihirisha zaidi, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mfumo thabiti unaoendana na wakati.

"Uwezo wa taasisi za fedha na utayari wa kukabiliana na changamoto wakati wote ni muhimu sio tu kwa utulivu na ustahimilivu wa uchumi, bali pia ni kwa ajili ya kudumisha ustawi wa jamii na siasa."

Gavana Tutuba amefafanua kuwa, pamoja na mada kuu, washiriki wa kongamano watapata fursa katika siku mbili zijazo kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mada tatu.

Miongoni mwa mada hizo ni ufanisi na uhimilivu wa taasisi za fedha wakati wa majanga. 

Amesema, wakati wa majanga au mikasa mbalimbali, taasisi za fedha zinakutana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ongezeko la mikopo chechefu (isiyolipika) na kupungua kwa mitaji na kuongezeka kwa gharama za fedha za kukopesha.

"Majadiliano chini ya mada hii yanatarajiwa kutoa mwanga kuhusu namna taasisi za fedha zilivyoweza kujikwamua na madhara ya majanga ya miaka ya hivi karibuni na jinsi taasisi hizo zinavyopaswa kujiweka tayari kujikinga na athari za majanga yanayoweza kutokea hapo baadaye."

Nyingine ni kuhusu uhimilivu wa sekta ya fedha katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi, jukumu la sheria mbalimbali, ubunifu na usimamizi wa vihatarishi.

Gavana Tutuba amesema, changamoto za hivi karibuni duniani, ubunifu na mabadiliko katika mifumo ya usimamizi wa vihatarishi kwa pamoja vinalazimisha marekebisho katika mfumo wa udhibiti ili kuhakikisha ustahimilivu wa sekta ya fedha.

Amesema, majadiliano kwenye eneo hili yanatarajiwa kujikita zaidi katika masuala ya ufanisi wa sheria na kanuni mbalimbali za kifedha, njia za ubunifu na mikakati imara inayoweza kuimarisha usimamizi wa vihatarishi katika ustahimilivu wa sekta ya fedha.

Vile vile, mada ya tatu itaangazia kuhusu ubunifu wa kiteknolojia katika utoaji wa huduma za kifedha: Kichocheo cha ustahimilivu.

Gavana Tutuba amesema, mada hii itabainisha ubunifu wa teknolojia mpya unatoa fursa kwa taasisi za fedha katika kuboresha utoaji wa huduma za fedha na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza.

"Kongamano hili linatarajiwa kutoa ufahamu zaidi kuhusu jinsi ya kutumia maendeleo ya kiteknolojia ili kujenga sekta imara ya fedha.

"Tunashukuru kuwa na watoa mada mashuhuri kutoka Tanzania, Zimbabwe, Kenya, Marekani, Bangladesh, na Nigeria ambao kwa umahiri wao naamini watazitendea haki mada hizo na baadaye kuja na mikakati ambayo itatusaidia ...watakaochangia mawazo na uzoefu wao."

Mbali na hayo, Gavana Tutuba amesema, licha ya changamoto za kiuchumi duniani, uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 4.8 katika kipindi cha miaka ya 2020 na 2022 kulinganishwa na wastani wa asilimia 2.3 wa nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara.

Pia, amesema, kati ya mwaka 2020 na 2023 mfumuko wa bei ulikuwa wastani wa asilimia 3.8, chini ya lengo la kati la nchi la asilimia 5.

Hali hii, Gavana Tutuba amesema, ilisababishwa kwa kiasi kikubwa na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti, pamoja na mageuzi ya kimuundo yanayoendelea nchini.

"Kama sehemu ya kuimarisha ufanisi wa sera ya fedha na kuendana na Itifaki ya Umoja wa Fedha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambayo inalenga kuwa na sarafu moja kwa kanda ifikapo mwaka 2031, mwezi Januari 2024 Benki Kuu ya Tanzania ilihama rasmi kutoka katika kutumia mfumo wa sera ya fedha unaotumia ujazi wa fedha na kuanza rasmi kutumia mfumo mpya unaotumia riba.

Hii inamaanisha kuwa katika kutekeleza sera ya fedha, Benki Kuu itakua ikitangaza riba ya Benki Kuu (CBR-Central Bank Rate) ambayo itakuwa ikitoa mwelekeo wa sera ya fedha katika kipindi cha robo mwaka.

"Ni matarajio yangu kwamba benki na taasisi nyingine za fedha zitatumia kiwango cha riba ya Benki Kuu kama kiashiria muhimu cha mabadiliko ya viwango vya riba kwa wateja wa taasisi hizo za fedha."

Amesema, pamoja na athari za mitikisiko mbalimbali ya uchumi wa dunia, sekta ya fedha ya Tanzania imebaki himilivu na imeendelea kuwa miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi hasa katika kipindi cha baada ya janga la UVIKO-19.

Aidha, sekta hii imeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa sera ya fedha na kurahisisha malipo nchini.

Mwaka 2022, sekta hii ilikua kwa asilimia 9.2 na kuchangia asilimia 6.6 kwenye ukuajia wa Pato la Taifa. Ukuaji huu ulikuwa bora ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.1 na mchango wa asilimia 2.2 mwaka 2020.

Pia, amesema sekta ya fedha imekuwa na ongezeko la huduma mpya za kifedha na mabadiliko ya mifumo ya utoaji huduma, ikisaidiwa na uvumbuzi na mabadiliko ya teknolojia.

Hadi sasa, miamala mbalimbali kama vile uhamishaji wa fedha, malipo ya ankara na kodi, pamoja na huduma nyingine inafanyika ndani ya muda mfupi kupitia mifumo ya kidigitali.

Hapo kabla, miamala hii ilikuwa ikifanyika nje ya mifumo ya kidigitali na hivyo kuchukua muda mrefu na kwa gharama kubwa.

"Kwa sasa, tunaendelea kuangalia namna ambayo matumizi ya mifumo hii ya kidigitali, kwa mfano huduma za malipo kwa njia ya simu za mkononi, yanaweza kuongezwa ili kuboresha uhimilivu wa kiuchumi na kifedha dhidi ya majanga."

RC

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda Mtaifikolo,amesema, “Wananchi wa mkoa wa Arusha wana imani kubwa sana na Serikali yao inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi nzuri inayofanya na inayoendelea kufanywa katika kuleta maendeleo kwa wananchi wote wa Tanzania.
“Pia, ninapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana waandaaji wa mkutano huu (BoT na TBA) kwa kutupa heshima kubwa, sisi wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa kutupa nafasi hii kubwa ya ku-host mkutano huu wa kifedha na mkutano huu muhimu sana kwa uchumi wetu nchini.

"Tunafahamu kabisa, Sekta ya Fedha ni muhimu sana na ili ikuwe lazima sekta binafsi nayo iendelee kukuwa, nichukue fursa hii kuishukuru sana Serikali kwa jitihada kubwa ambazo zinaendelea kufanyika chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan za kuchochea maendeleo ya Sekta ya Fedha na ukuaji wa uchumi nchini."

Amesema, Serikali imejidhatiti kuweka mazingira wezeshi ya kuimarisha ukuaji wa uchumi ikiwemo sekta ya fedha hasa nyakati hizi zenye changamoto za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuweka sera nzuri na ushirikishaji ambazo zinafanya sekta binafsi ikuwe kwa haraka.

Sabi

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki Tanzania (TBA),Theobaid Sabi amesema,mkutano huu ni muhimu sana katika Sekta ya Fedha nchini.
“Kauli mbiu ya kongamano hili la 21 ni Kuimarisha Ustahimilivu wa Sekta ya Fedha Nyakati za Changamoto za Kiuchumi, ukizingatia hali ya uchumi duniani, hasa kupanda kwa riba kwenye masoko ya kifedha duniani.

"Vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi, vita inayotishia kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali kama vile mafuta ya Petroli zikiwemo athari nyingine za kiuchumi, majanga yaliyotokana na janga la UVIKO-19 na chanagamoto zingine za kibiashara duniani ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi na changamoto za kiteknolojia hususani uhalifu wa kimtandao ni baadhi ya changamoto zinazotukabili kwenye sekta ya fedha hapa nchini, lakini hasa ni changamoto zinazoikabili dunia nzima.

“Changamoto hizi zimeendelea kuleta athari nyingi kwenye sekta ya fedha duniani na hapa nchini, Mheshimiwa Makamu wa Rais ni wazi kwamba changamoto hizi zitaendelea kuwepo duniani, lakini kama wanavyosema Wahenga bahari tulivu haipimi nahodha wa meli ni katika nyakati kama hizi ambapo sisi tuliopo kwenye sekta ya fedha tunapaswa kuja na majibu ya changamoto hizi.

"Hivyo basi, wakati ambapo Sekta ya Fedha duniani inapitia majaribu, kwetu ni muda sahihi kukutana, kuchangia mawazo ili kwa pamoja tuweze kubuni mbinu za kukabiliana na changamoto hizi, kwa hivyo kupata fursa ya kukutana kwenye kongamano hili ni jambo la kutia moyo sana kwenye sekta ya fedha.

Amesema, “Mwelekeo wetu kwenye umoja wa mabenki ni kuendelea kukabiliana na changamoto hizi ili kupunguza athari za majanga na hivyo kuziwezesha sekta muhimu kama vile kilimo, viwanda, utalii na pia wajasiriamali wadogowadogo waaendelee kustawi.

"Jukumu letu katika kuwezesha wananchi kiuchumi tunaendelea kulitekeleza na tunajivunia ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi, ongezejo ambalo kufikia Desemba, mwaka 2023 ulifikia asilimia 17.1."

Sabi amesema, mabenki yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya Sekta ya Fedha hapa nchini. "Na tukirudi nyuma tukiangalia wakati wa janga la UVIKO-19 mabenki nchini kwa ujumla yalichukua hatua za makusudi kuweka masharti yaliyokuwa rafiki ili kuwawezesha wakopaji na wananchi kwa ujumla walioathirika hasa kwenye sekta kama vile ya utalii na malazi na pia usafirishaji kuweza kumudu kipindi kile kigumu.

"Mabenki yaliweka masharti nafuu, masharti ambayo yamepelekea wakopaji wengi kwenye sekta kama vile utalii kuweza kukopa na kuhimili kipindi kile cha Uviko."

Pia, amesema ni imani yao kwamba pale patakapojitokeza hali ngumu, mabenki yataendelea kuingilia kati kwa kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha sekta za uzalishaji zinapata ahueni inayohitajika.

"Benki zinaendelea kuchukua hatua, kuongeza wigo wa kupatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi walio wengi kama huduma jumuishi za kifedha. Kwa ripoti za mwaka 2023 Financial Inclusion kwa sekta ya fedha ilikuwa kwa asilimia 22 ikiwa imeongezeka kutoka asilimia 17 mwaka 2017.

"Ongezeko hili, ni matokeo ya juhudi mbalimbali za makusudi za Serikali, za Benki Kuu ya Tanzania, na mabenki hapa nchini, tubakubali kwenye sekta ya mabenki kwamba ujumuishi huu wa asuilimia 22 bado ni mdogo tunazielekeza kuendeleza ujumuishi huu.

Vile vile amesema, wanaendelea kutoa elimu ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu mikopo ambayo watakopa iweze kuwawezesha kwenda kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

"Mabenki yanaendelea kutoa elimu kuhusu ufahamu juu ya fursa za kifedha hasa fursa za mikopo ili wananchi wengi waweze kufaidika na hduma rasmi za mikopo na hivyo waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi nchini."

Katika hatua nyingine, kwa niaba ya sekta ya mabenki nchini, Sabi ameendelea kuishukuru Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi na bora ambayo yanawawezesha kutekeleza mipango yao kikamilifu ili kuhakikisha sekta ya fedha inapiga hatua nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news