DAR ES SALAAM-Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015.
Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.
Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995.
Ni ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya. Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)