NA FRESHA KINASA
KATA ya Musanja iliyopo katika halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara yenye vijiji vitatu haina Kituo cha Afya na haina zahanati hata moja kwenye vijiji vyake. Vijiji hivyo ni Mabuimerafuru, Musanja na Nyabaenge.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Jimbo la Musoma Vijijini Machi 23, 2024.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, hiyo ndiyo kata pekee jimboni yenye hali kama hiyo kwa upande wa huduma za afya.
"Wanavijiji wa kata hii wanalazimika kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 10 kwenda kupata huduma za afya kwenye kata jirani ya Murangi (Kituo cha Afya cha Murangi),"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,Zahanati ya Kijiji cha Nyabaengere inakaribia kuanza kutoa huduma za afya. Maombi ya kufungiwa umeme yamepelekwa TANESCO.
Taarifa hiyo imesema kuwa, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo aliendesha harambee ya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji Cha Mabuimerafuru siku ya Jumatano Machi 20, 2024.
Ambapo matokeo ya harambee hiyo, fedha zilizopatikana ni Shilingi 1,350,000, Saruji Mifuko 59, Kondoo 2,
Ambapo Mbunge wa Jimbo Prof. Sospeter Muhongo alitoa saruji mifuko 200. Huku Kamati ya Ujenzi iliundwa chini ya uongozi wa Justine Joshua.
Viongozi wa CCM wa Kata na Matawi, na baadhi ya wananchi wa Kata ya Musanja walipewa vitabu viwili viwili vinavyoelezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025 ndani ya vijiji vyote 68 vya jimbo hilo.
Aidha, taarifa hiyo imeelekeza kuwa michango kutoka kwa wadau wa maendeleo wa Kata ya Musanja unapaswa ufanyike kwa kutuma fedha za michango moja kwa moja kwenye Akaunti ya Kijiji.
Ambayo ni Benki, NMB, Akaunti Namba 30310037402, Jina: Kijiji cha Mabuimerafuru.