MANYARA-Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara imemhukumu, Ramadhani Rashid Msangi ambaye aliwahi kuwa Mshauri wa Wafanyabiashara mwajiriwa wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) mkoani Manyara.
Ramadhani ameamriwa kulipa faini kiasi cha shilingi 900,000 au kwenda jela miaka mitatu, kwa kosa la kughushi nyaraka za malipo.
Hukumu hiyo dhidi ya Ramadhani Rashid Msangi katika shauri la uhujumu uchumi Na. 05/2023, imetolewa Machi 22,2024 chini ya Mhe. Martin Massao, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Manyara.
Ilidaiwa mshtakiwa alighushi nyaraka mbalimbali katika marejesho yake kuonesha kuwa alihudhuria na kuendesha mafunzo ya wajasiriamali yaliyofanyika wilayani Hana'ng kwa kipindi cha mwezi Februari na Juni mwaka 2018.
Katika kipindi hicho inadaiwa alitumia kiasi cha shilingi 6,695,000 kugharamia posho ya chakula, ukumbi na nauli kwa waliodaiwa kushiriki mafunzo hayo huku akijua taarifa hizo hazikuwa sahihi.
Aidha,mshitakiwa amelipa faini na kuachiwa huru na Mahakama.