RUVUMA-Watu tisa wamefariki dunia katika kijiji cha Lumeme Halmashauri ya Nyasa mkoani Ruvuma baada ya gari walilokuwa wanasafiria aina ya Noah lenye namba za usajiri T795 BIS kusombwa na maji kwenye mto Kisimani.
Gari hilo lilikuwa limetoka katika kijiji cha Tingi wilayani Nyasa kuelekea kijiji cha Lumeme majira ya saa 12 jioni Machi 11,2024.
Diwani wa Kata ya Lumeme Mheshimiwa Walarick Ndunguru amesema katika ajali hiyo watu wanne wamenusurika huku watu tisa wakipoteza maisha.
Diwani huyo amesema ajali hiyo imechangiwa na uzembe wa dereva ambaye alitakiwa kusubiri maji yapungue kwenye kivuko cha Mto Kisimani ndipo avuke.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Jumanne Mwankhoo kwa niaba ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ametoa pole kwa wafiwa na wananchi wa kata ya Lumeme.
Ametoa rai kwa madereva kuwa makini wanapoendesha vyombo vya usafiri hasa katika kipindi hiki cha mvua za masika ili kuepusha madhara.
Mwakilishi wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma,Mhandisi Anselim Chambila amesema watarajia kufanya matengenezo makubwa kwenye kivuko kilichopo katika mto Kisimani mara baada ya kupungua kwa mvua za masika.
Kamanda wa polisi Mkoani Ruvuma, SACP Marco Chilya amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.