OUT yawapa heko wanawake wa Tanzania

NA DKT.MOHAMED OMARY MAGUO

CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kinawapongeza wanawake wote wa Tanzania kutokana uwajibikaji wao mkubwa katika kazi na kujitoa kwao katika malezi ya familia na kujenga taifa imara la Tanzania.
(Picha na Maktaba/Jamhuri)

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Prof. Elifas Tozo Bisanda wakati wa kikao cha Kamati Tendaji ya Baraza la Wafanyakazi wa OUT lililoketi tarehe 08 Machi, 2024 Kinondoni jijini Dar es Salaam. 

Kando ya mkutano huo Prof. Bisanda alizungumza na Kitengo cha Mawasiliano na Masoko cha OUT na kueleza:

"OUT tunawapongeza sana wanawake wote na kuwatakia heri katika siku hii adhimu ya kusherehekea siku ya mwanamke duniani. Wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa na jamii yetu kwa jumla.

"OUT tunajivunia kuwa na watumishi wanawake ambao wanatimiza majukumu yao vizuri kwa ufanisi wa hali ya juu na kuleta tija kwa Taasisi yetu.

"Tunafahamu majukumu ya wanawake katika jamii na hususani katika familia ni makubwa lakini bado wawapo katika majukumu ya kazi hutekeleza kikamilifu bila ajizi,"amesema Prof. Bisanda.

Aidha, ameongeza kwamba anawahimiza wanawake wote wa Tanzania kuhakikisha wanashirikiana baina yao na pia wanashirikiana na wanaume katika kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo kwa Taifa na jamii kwa jumla.

Ushirikiano ndiyo nguzo muhimu katika kuleta maendeleo kwenye jamii na mahali pa kazi, biashara, kilimo, ufugaji na ujasiriamali.

Naye, Naibu Makamu wa OUT anayesimamia Taaluma, Tafiti, na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Deus Ngaruko amewapongeza wanawake kwa kusherehekea vizuri siku ya wanawake duniani na kuwataka kujiendeleza kielimu kupitia OUT huku wakiwa wanaendelea na majukumu yao. .

"Wanawake ni watu waliobanwa sana na majukumu ya kifamilia, kijamii, kikazi na uchakarikaji katika mambo ya ujasiriamali mdogo, wa kati na mkubwa na wakati huo huo ni walezi wakubwa wa familia.

"Hakika OUT ndipo mahala sahihi kwa wao kujiendeleza kielemu huku wakiendelea na majukumu yao.

"Chuo chetu kinatoa fursa pana kwa watu wote wenye majukumu na kwa upande wa wanawake wanaweza kabisa kusoma kwetu bila kuathiri mipango yao ya uzazi, malezi ya watoto na familia pamoja na shughuli za utafutaji wa riziki na ujenzi wa Taifa,"amesema Prof. Ngaruko.

Aidha, ameongeza kwamba kutokana na mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji iliyopo OUT wanawake hujiendeleza vizuri wakiwa sambamba na familia zao kwa kuziangalia kwa karibu kila siku.

Jambo hili ni kubwa na linatoa fursa kwa wanawake wote kutokuona wajibu wao wa malezi ya watoto na familia kama kikwazo cha wao kujiendeleza kielimu katika ngazi za astashahada, stashahada, Shahada za kwanza, shahada za umahiri na uzamivu.

Kwa upande wake, Naibu Makamu wa Chuo anayeshughulikia Huduma za Mikoa na Teknolojia za Kujifunzia Prof. Alex Makulilo ameeleza kwamba, OUT ina vituo katika mikoa yote ya Tanzania Bara, Kahama na Tunduru, vituo vya uratibu Tanzania Zanzibar- Unguja na Pemba.

Pia, kuna vituo vya mitihani katika wilaya mbalimbali nchini. Lengo lake kubwa ni kuwafikia wanafunzi wakiwepo wanawake kule kule walipo wajiendeleze kielimu huku wakitimiza majukumu yao ya ujezi wa Taifa. Amesema Prof. Makukilo,

"Hongereni sana wanawake wote katika kusherehekea siku hii adhimu ya wanawake duniani. Sisi OUT tunafahamu majukumu mazito mliyonayo katika jamii na hivyo, tumesogeza huduma karibu kabisa ili msipate vikwazo vya kujiendeleza kielimu. 

"Tumieni fursa za kujiunga na OUT muweze kutimiza ndoto zenu za Elimu mkiwa huko huko mlipo mijini na vijijini mkifanya kazi katika sekta binafsi na sekta ya umma."

Mintaarafu ya hayo, Prof. George Oreku ambaye ni Naibu Makamu wa OUT anayesimamia Fedha, Mipango na Utawala amewapongeza sana wanawake na kuhitimisha kwa kauli mbiu ya mwaka huu inayosema 

"Wekeza kwa Wanawake; Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii." na akaongeza maneno "Heko kwa Wanawake wote katika kusherehekea siku ya Wanawake duniani."

Wanawake wote Hoyeeeeeeeeeeeeeeee!!!!!

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news