NA DKT.MOHAMED MAGUO
CHUO Kikuu Huria cha Tanzania kimejipambanua kwa sifa ya ubunifu katika maeneo mbalimbali na kuendelea kukifanya kuwa Chuo Kikuu bora kinachotoa Elimu ya juu kwa njia ya Huria, Masafa na Mtandao kati ya vyuo Vikuu Huria 120 duniani.
Hayo yamesemwa na Prof. Deus Ngaruko alipokuwa akifunguwa mafunzo ya "Ulinzi wa Miliki Ubunifu" kwa maafisa wa OUT mjini Bagamoyo tarehe 11/03/2024. Prof. Ngaruko anaeleza kwamba,
"OUT ni Taasisi ya Elimu ya juu ambayo kwa kweli imekuwa ikikuza ubunifu katika maeneo mbalimbali ya TEHAMA, uongozi, menejimenti, mifumo ya mitihani, mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji, shughuli za mawasiliano ma masoko, huduma kwa jamii na uwajibikaji wa taasisi kwa jamii.
"Ubunifu huu umeijengea OUT heshima kubwa kutokana na kusaidia kutatua changamoto za jamii kwa haraka na kuleta ustawi," amesema Prof. Ngaruko.
Kutokana na ubunifu huu taasisi mbalimbali za ndani na nje zimekuwa zikipenda kutumia bunifu za OUT kwenye taasisi zao na jambo hili linatusukuma kuhakikisha kuwa tunakuwa na uwezo na utaalamu wa Ulinzi wa Miliki Ubunifu.
Hii ndiyo sababu kubwa ya kufanya mafunzo haya ambayo yanatolewa na wataalamu kutoka BRELA, COSOTA na COSTECH kwa siku tatu. Prof. Ngaruko ameongeza,
"Ubunifu wetu wa mfumo wa mitihani ya kuongea (OREX) umezivutia taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ikiwemo Shanghai Open University na kutaka kuanza kuutumia katika chuo chao.
"Mfumo huu tuliubuni katika kipindi cha CORONA ambapo wanafunzi walifanya mitihani yao wakiwa huko huko walipo kwa ubora wa hali ya juu kabisa.
"Mfumo kama huu na mingine tunahitaji kuwa na Ulinzi wa Miliki ubunifu ili wote wanaopenda basi wafuate utaratibu kuupata.
"Mfumo wetu wa mitihani kwa jumla hapa OUT ni bullet proof ambapo si mwalimu wa somo wala mkuu wa idara au kitivo anayeweza kufahamu maswali yatakayokuwa kwenye mtihani.
"Kila kitu kinafanywa na mfumo na mitihani hurudufishwa dakika 30 kabla mtihani haujafanyika. Hili huwezi kukipata popote isipokuwa OUT. Leo taasisi kadhaa zinataka mfumo huu kutoka kwetu," amesema Prof. Ngaruko.
Ubunifu huu ni sehemu tu kati ya bunifu nyingi ambazo zinafanyika OUT na mafunzo yanayotolewa ni muhimu sana kwa wadau wote wa chuo wanaohusika na masuala ya ubunifu.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza la OUT ambaye pia ni mwanasheria wa Chuo, wakili Nelly Moshi ameyazungumzia mafunzo hayo kuwa yamekuja wakati muafaka na kitengo cha sheria cha Chuo kinashiriki kikamilifu ili kuweza kukiongoza na kukishauri Chuo vizuri kabisa katika eneo la Ulinzi wa Miliki Ubunifu. Amefafanua zaidi,
"Chuo chetu kimekuwa na utajiri mkubwa sana wa bunifu nyingi zenye viwango vya hali ya juu na zinakiletea sifa chuo chetu. Tutahakikisha tunajizatiti kwenye Ulinzi wa Miliki Ubunifu ili kama taasisi tuweze kunufaika kwa mawanda mapana zaidi na bunifu za OUT," amesema wakili Nelly Moshi.
Naye, Mkurugenzi wa Utafiti, machapisho na Uvumbuzi wa OUT Dkt. Harrieth Mtae ameishukuru Menejimenti kwa kuwezesha mafunzo haya muhimu kabisa ya kuwajengea watumishi uwezo katika eneo la Ulinzi wa Miliki Ubunifu hasa katika kipindi hiki ambapo taasisi imekuwa na bunifu nyingi zenye kuleta tija kwa taasisi, jamii na taifa kwa jumla. Dkt. Mtae amesema,
"Bunifu za OUT ni za kiwango cha hali ya juu sana na kama itakumbukwa bunifu mbili zilishinda nafasi ya juu kwenye mashindano ya MAKISATU ya mwaka 2022 na kupata tuzo. Hii ni ushahidi tosha kwamba OUT ni kitovu cha ubunifu," meongeza Dkt. Mtae.
Mafunzo hayo yameanza tarehe 11 Machi, 2024 na yanatarajiwa kukamilika tarehe 13 Machi, 2024. Washiriki wametakiwa kufuatilia mafunzo hayo kwa makini na kujenga uwezo uliokusudiwa Kwa lengo la kuiwezesha OUT kunufaika na ubunifu unaofanywa na watumishi wake.