SONGWE-Serikali ya Awamu Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetekeleza ombi la siku nyingi la wachimbaji wadogo wilayani Songwe.
Ni kwa kuwatengea eneo la uchimbaji na kuwakabidhi jumla ya Leseni ndogo 37 zilizopo eneo la Kata ya Saza kutoka Leseni hodhi namba RL0009/2014 ya iliyokuwa Kampuni ya Bafex Tanzania Limited.
Hayo yameelezwa leo Machi 23, 2024 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde alipofika eneo la Saza Wilayani Songwe kukabidhi leseni 19 kwa wachimbaji wadogo wa Kikundi cha Songwe Gold Family (SGF) na wachimbaji wengine wadogo wadogo 18 huku mchakato wa kuendelea kutoa Leseni zaidi ukiendelea.

Waziri Mavunde amesema pamoja na kwamba wachimbaji hao wanachimba kwa kubahatisha, kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Februari, 2024 wamezalisha kilo 729.6 zenye thamani ya shilingi bilioni 101.06 na kueleza kuwa anaamini kwa kupatiwa leseni hizo hawatomwongusha Mhe. Rais kwa kuongeza uzalishaji na mapato yatokanayo na madini.
Pia, Mhe. Mavunde amebainisha kuwa, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha inaondoa ujanja ujanja kwenye shughuli za uchimbaji madini ambapo tayari imekwishatangaza kufuta jumla ya leseni na maombi 2,648 ambazo hazijaendelezwa na zimekiuka taratibu za umiliki wa leseni za madini.
Mhe. Mavunde ameendelea kusisitiza kwamba hatasita kuendelea kufuta leseni kwa wamiliki wote ambao wanakiuka taratibu za umiliki wa leseni za madini, ambapo ametoa mfano wa uwepo wa baadhi ya watu 6 tu wanaomiliki leseni zenye ukubwa wa zaidi ya ekari milioni 13.

Awali, akisoma risala kwa Waziri Mavunde, Mwenyekiti wa Kikundi cha Wachimbaji wadogo cha Songwe Gold Family (SGF), Bw.Simon Ndaki amebainisha kwamba Kikundi chao kiliomba siku nyingi maeneo ya kuchimba na kupelekea kushindwa kuwekeza mitaji mikubwa kutokana na kukosa uhakika wa maeneo.
"Tunaahidi sasa kwamba tunakwenda kuwekeza mitaji mikubwa na kuhakikisha tunaongeza mchango zaidi wa mapato ya halmashauri na Pato la Taifa kwa ujumla," amesema Ndaki.
Akieleza kuhusu masuala mbalimbali ya Wilaya ya Songwe, Mbunge wa Jimbo la Songwe,Mhe. Philipo Mulugo amwishukuru Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutatua changamoto hiyo iliyodumu kwa muda mrefu na kumwomba Waziri Mavunde kupeleka shukrani za wachimbaji wadogo kwa Mhe. Rais na kueleza kwamba wapo tayari kusaidia kurejesha fedha zaidi ya bilioni 72 zilizolipwa Bafex Tanzania Limited kwa uzalishaji mkubwa wa dhahabu.
