RC Mtanda ampa neno Rais wa TCCIA

NA FRESHA KINASA

MKUU wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Said Mohamed Mtanda amemhakikishia Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA),Vicent Minja kuwa serikali ya mkoa huo itaendelea kuimarisha mazingira mazuri, wezeshi na kushirikiana na sekta binafsi kikamilifu ili kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara wengi kuja kuwekeza mkoani humo.
Mheshimiwa Mtanda ameyasema hayo leo Machi 22, 2024 wakati akizungumza na Rais wa chemba hiyo ofisini kwake Mjini Musoma alipofanya ziara mkoani humo ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara yake mikoa mbalimbali hapa nchini.

Mtanda amesema kuwa, sekta binafsi ni muhimu katika maendeleo ya uchumi wa nchi,hivyo serikali ya mkoa imejidhatiti vyema kushirikiana na sekta binafsi kuona fursa zote za kiuchumi ambazo zipo ndani ya Mkoa huo zinatumiwa kikamilifu kubadilisha maisha ya Wananchi na kuchangia maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Amesema, hivi Sasa Mkoa wa Mara hali ya usalama imeimarika kutokana na kupungua kwa matukio ya kihalifu ambayo awali yalikuwepo kwa kiasi kikubwa ikiwemo wananchi kuvamia maeneo ya wawekezaji migodi.

Hali ambayo ilikuwa inawafanya baadhi ya wawekezaji kuogopa kuja kuwekeza ndani ya mkoa huo, lakini kwa sasa hali ni shwari hivyo wawekezaji waje kwa wingi mkoani humo.

Pia amesema kuwa, Serikali inaendelea na ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Musoma ambao unagharimu fedha zaidi ya Bil. 35 kwa sasa ujenzi umefikia asilimia zaidi ya 58. Ambapo ukikamilika amesema matarajio ni makubwa katika kuinua uchumi wa mkoa wa Mara kupitia watalii ambao watatua na ndege kuja kutalii hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Amewataka pia Wafanyabiashara wakubwa wa Mkoa wa Mara kujenga hotel kubwa za kisasa ambazo zitahifadhi wageni kutoka mataifa mbalimbali. Na Mkoa umejipanga vyema kuitangaza hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuwa ipo Mkoani Mara ili iwanufaishe Wananchi wa Mkoa huo na kuufungua Mkoa kiuchumi.

"Wafanyabiashara wasikimbie kuwekeza ndani ya Mkoa wa Mara, waje wawekeze nyumbani. Serikali imeendelea kuboresha mazingira mazuri kila siku tunahitaji kuujenga Mkoa kwa pamoja na tuzidi kushirikiana waliokwenda kuwekeza nje ya Mkoa warudi kuwekeza hapa,"amesema Mheshimiwa Mtanda.

Amesema kuwa katika kuwatumikia Wananchi, serikali ya Mkoa imeendesha Kliniki ya ardhi maeneo mbalimbali na imesaidia utatuzi wa migogoro ya ardhi ipatayo 1,800. Ambapo migogoro iliyobakia ni 200 ambayo inahitaji Mamalaka za juu. Huku akisema kwa Sasa Mkoa utaendesha Kliniki katika Vijiji vinavyopakana na maeneo ya migodi ili kujenga Mahusiano mema na kutatua changamoto za wananchi.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara, Kilimo na Viwanda Boniphace ndengo amesema kuwa TCCIA kimekuwa chombo muhimu cha kuwaleta Wafanyabiashara, wajasiriamali, wabunifu na wavumbuzi wa fursa mbalimbali pamoja na kitaendelea kuwaunganisha kusudi kuweza kukuza mawazo yao, fikara na njozi walizonazo kibiashara wapige hatua.

Amesema kuwa chombo hicho kilishiriki vyema katika kuandaa mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa huo ambao ulizinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa miata mitatu iliyopita Jambo ambalo liliimarisha Mahusiano mazuri baina ya TCCIA na Serikali ya Mkoa wa Mara.

Naye Rais wa TCCIA Nchini Vicent Minja amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Said Mtanda kwa muda ambao amekuwepo amekuwa karibu na sekta binafsi katika kushirikiana nayo.

Pia, amemuomba Mkuu wa Mkoa huo kuwahimiza Wafanyabiashara wajiunge na TCCIA pamoja na kushirikiana na TCCIA katika masuala mbalimbali ambayo yanafaida kwa uchumi wa Wananchi wa Mkoa huo ikiwemo kutangaza fursa zilizomo Mkoani Mara kitaifa na kimataifa.

Pia amesema kuwa iwapo Wafanyabiashara watajiunga katika chemba hiyo itakuwa rahisi kuwaunganisha na fursa mbalimbali ambazo chemba inakusudia kuzifanya kwa wafanyabiashara ikiwemo mikopo kutoka benki ya maendeleo ya Kilimo TADB na kuelimishwa masuala muhimu ya kibiashara na uwekezaji.

Aidha, akizungumza na Wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara katika Ukumbi wa uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkoa wa Mara Minja amewataka Wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara kushikamana na kuwa na umoja. Huku akisema changamoto mbalimbali zinazowakabili zitaendelea kufanyiwa kazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news