NA VERONICA SIMBA
REA
WALIMU na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Chekelei iliyopo kijiji cha Madumu, wilayani Korogwe, Mkoa wa Tanga wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wanapata huduma zote za msingi ikiwemo umeme na vitendea kazi mbalimbali, hali ambayo wameeleza itasaidia kuboresha taaluma shuleni hapo.
Wametoa shukrani hizo leo Machi 26, 2024 wakati Bodi ya Nishati Vijijini (REB) na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) walipotembelea Shule hiyo na kukabidhi Printa ya kisasa, wino wake pamoja na karatasi za kuchapishia, ikiwa ni kutimiza ahadi iliyotolewa Machi mwaka jana na aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Akizungumza mbele ya Ujumbe huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, Mkuu wa Shule, Siwema Mashoto amesema uwepo wa umeme wa REA sambamba na Mashine hiyo ya Printa waliyokabidhiwa pamoja na vifaa vyake vitasaidia kuboresha kiwango cha elimu kwa wanafunzi.
“Hakika Mama Samia anaupiga mwingi na REA mmemheshimisha. Tunamshukuru sana. Baaada ya muda rudini mtuulize kuhusu mabadiliko katika kiwango cha taaluma maana tunaamini yatakuwa yamekuwa bora zaidi,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi Balozi Kingu amewataka walimu na wanafunzi kutunza vyema vifaa walivyopatiwa na kuvitumia kwa tija ili vilete manufaa yanayokusudiwa kwao.
Awali, akieleza lengo la ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa REA ambaye pia ni Katibu wa Bodi, amesema Wakala unatamani kuona wananchi wote waliofikiwa na umeme wanautumia kwa tija ili azma ya Serikali inayolenga kuboresha maisha vijijini itimie.
“Ndiyo maana leo tumewatembelea ili kutekeleza ahadi iliyotolewa kwenu na viongozi wetu. Tunataka wananchi waelewe kwamba kuunganisha umeme peke yake haitoshi ikiwa hautumiki kubadili maisha. Printa na vifaa vingine tulivyowapatia leo, vinalenga kuleta tija ya uwepo wa umeme shuleni hapa,” amefafanua.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu ametoa ahadi kuwa REA itawapatia majiko banifu, Walimu wote wa Shule hiyo pamoja na viongozi mbalimbali walioshiriki katika tukio hilo ili wawe Mabalozi wazuri wa Ajenda ya Rais Samia ya kumtua Mama kuni kichwani kwa kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Pia, ameahidi kuwa REA itakamilisha kazi ya kutandaza mfumo wa nyaya za umeme (wiring) katika majengo yote ya shule hiyo ili umeme ambao umekwishafikishwa utumike kwa tija zaidi.
“Tutatuma wataalamu kufanya tathmini kisha tufanye hiyo kazi mara moja.”
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi, Kata ya Chekelei, Mohamedi Fumbili ameipongeza Serikali kupitia REA akinukuu maneno kutoka Vitabu Vitakatifu kuwa ‘anayeahidi na kutimiza anapata thawabu kwa Mungu.”
Aidha,ameongeza kuwa tukio lililofanywa na REA ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala hivyo ni kumuheshimisha Mwenyekiti wake, Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali kwa ujumla.
Bodi ya Nishati Vijijini iko mkoani Tanga kushiriki vikao vya kazi na hivyo inatumia fursa hiyo pia kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini.