ZANZIBAR-Rais wa Rotary Club ya Zanzibar Stone Town,Augustine Mwombeki ameishauri jamii kuwa na tabia ya kuchunguza afya mara kwa mara ili kugundua magonjwa nyemelezi na kupata tiba mapema.

Amesema, uwepo wa kambi za uchunguzi na matibu vijijini kunahamsisha na kushajihisha wananchi kujitokeza kuchunguza afya zao na kuishauri jamii kuchangamkia fursa za kambi hizo pale zinapotokezea.
Aidha, alizitaka taasisi nyingine za Serikali na binafsi kushirikiana kujidhatiti kutoa huduma bora za afya kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuunga mkono kambi kama hizo ziweze kufanyika mara kwa mara vijijini, kwani wamekuwa wazito kwenda hospitali na kuishia kutumia mitishamba jambo ambalo linahatarisha afya zao.
Amefafanua kuwa, kambi hiyo ni kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa maradhi mbalimbali kwa watoto, wazee na kina mama wapatao 1,500 ambapo wamejipanga kutoa huduma tofauti zikiwemo uchunguzi wa magonjwa ya meno,macho,ngozi,masikio, koo na pua, HIV pamoja na magonjwa ya kina mama katika kijiji hicho.