Sekta ya Fedha ina mchango mkubwa nchini-Makamu wa Rais

NA GODFREY NNKO

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Mpango amesema, Sekta ya Fedha nchini imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi na maendeleo.
"Kwa sababu hiyo, napenda kutoa pongezi kwa kazi nzuri iliyofanywa na uongozi mahiri wa taasisi zote za sekta ya fedha nchini kwa kufanya sekta hii kuwa imara na himilivu.

"Ni kwa kuongeza ubunifu na uwezo wa kubadilika kuendana na mazingira yaliyopo. Hakika, mmesaidia kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi na maendeleo;

Dkt,Mpango ameyasema hayo leo Machi 7, 2024 wakati akifungua Kongamano la 21 kwa Taasisi za Fedha (COFI) katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Kongamano hilo ambalo linaongozwa na kauli mbiu ya "Kuimarisha Ustahimilivu wa Sekta ya Fedha Nyakati za Changamoto za Kiuchumi" limeandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Mabenki Tanzania (TBA).

Amesema, idadi ya watu wanaotumia huduma rasmi za fedha nchini iliongezeka hadi kufikia asilimia 76 mwaka 2023 kutoka asilimia 65 mwaka 2017.

Makamu wa Rais Dkt.Mpango amesema, hiyo ni hatua kubwa ambayo sote tunapaswa kujivunia. "Aidha, mikopo iliyotolewa na benki kwa sekta binafsi imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha baada ya UVIKO-19.

"Kwa mfano kwa mwaka 2022 na 2023, ukuaji wa mikopo ulifikia wastani wa asilimia 19.8 ikilinganishwa na asilimia 6.6 katika miaka miwili iliyotangulia.
"Halikadhalika, uwiano wa mikopo kwa sekta binafsi na Pato la Taifa ulifikia wastani wa asilimia 18.2 katika mwaka 2021-2022 ikilinganishwa na 17.6 mwaka 2020.

"Hata hivyo, uwiano huu ulikuwa chini ya wastani wa asilimia 26.6 kwa nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, hii inaashiria kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kama wadau wa sekta ya fedha.

"Ninatambua kuwa kongamano hili limekutanisha wataalamu wa sekta ya fedha wa Tanzania na wa kimataifa.

"Ninaamini kuwa maazimio ya majadiliano ya kongamano hili yatakuwa na mchango mkubwa katika kuandaa na kutekeleza sera, sheria, na kanuni zinazochochea maendeleo na uimara wa sekta ya fedha nchini."

Dkt.Mpango amesema, uimara wa sekta ya fedha unahitaji jitihada mbalimbali zinazojumuisha ushirikiano na ubunifu.

"Hivyo, usimamizi na udhibiti wa benki na taasisi za fedha ni msingi wa sekta ya fedha iliyo imara. Kama nchi na wataalamu tunapaswa kutoa kipaumbele katika eneo hili kuhakikisha utulivu na ustahimilivu katika sekta ya fedha, hasa katika kipindi cha changamoto za kiuchumi."

Pia, amesema soko la mitaji lililoendelea na lenye ufanisi linaweza kutumika kama kinga wakati wa changamoto za kiuchumi.

Dkt.Mpango amesema,ni muhimu kuwa na mikakati ya kuimarisha soko la mitaji, kulifanya liwe rahisi kufikiwa na kuvutia wawekezaji.
"Kuyumba kwa masoko ya kimataifa, upatikanaji hafifu wa mitaji na ongezeko la madeni, kunakochangiwa na migogoro ya kisiasa na mabadiliko ya tabianchi, vinaendelea kudhoofisha ukuaji katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.

"Hivyo basi, kuna haja ya kutumia vyema rasilimali fedha kwenye sekta binafsi, na kuboresha usimamizi wa fedha za umma pamoja na kupata suluhisho la ufadhili wa miradi ya maendeleo ya muda mrefu.

"Upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi. Hata hivyo, gharama ya mikopo katika soko la Tanzania bado iko juu, na siyo rafiki kwa ukuaji wa uchumi.

Pia, amesema,kongamano hilo linapaswa kutoa mapendekezo ya njia za kupunguza gharama za mikopo na huduma nyingine za fedha nchini hasa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.
Aidha, amesema hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuzuia madhara yake ni muhimu kwa uimara wa sekta ya fedha.

"Kwa hiyo, kuna haja ya kuendelea na kutekeleza hatua mbalimbali za kudhibiti madhara ya mabadiliko ya tabianchi zinazoendana na mazingira yetu.

"Ukuaji wa kasi wa teknolojia umebadilisha shughuli za sekta ya fedha, ukileta ufanisi na urahisi ingawa una changamoto kadhaa, ikiwemo hatari za usalama wa mtandao.

"Tunapaswa kuimarisha juhudi za kupunguza au kuepuka kabisa madhara yanayoweza kujitokeza, ikiwa ni pamoja na utunzaji wa siri wa taarifa, usalama wa mtandao, udhibiti wa fedha haramu, na kuwalinda watumiaji. Mambo haya yanatakiwa kwenda sambamba na ushirikishwaji wa wadau wote."

Wakati huo huo, Dkt.Mpango amewataka washiriki wa kongamano hilo kutafakari kwa kina changamoto ya uhaba wa fedha za kigeni uliopo kwa sasa na hatua za kuchukua kwa muda mfupi.

Amesema, kongamano hilo lijadili nafasi ya ubadilishanaji fedha katika udhibiti wa uhaba huo wa fedha za kigeni.

Amesema, kongamano hilo limekuja wakati mwafaka kwa kuzingatia kuwa hivi sasa dunia inakabiliwa na misukosuko ya kiuchumi na kijamii, hasa kufuatia kuvurugika kwa mifumo ya usafirishaji bidhaa ugavi na huduma kutokana na migogoro ya kisiasa kikanda na vita.

Sambamba na kasi kubwa ya maendeleo ya TEHAMA na mabadiliko ya tabianchi, ambavyo vyote vimegusa afya na mwenendo wa sekta ya fedha duniani.

Makamu wa Rais amesema,sekta ya fedha, ambayo inastahamili misukosuko ya kiuchumi ni muhilimili imara wa kiuchumi unaokuwa haraka, ambapo watalaamu bobezi katika masuala ya fedha waliopo ukumbini na nje ya ukumbi wanafahamu vizuri sifa ya sekta ya fedha yenye uwezo wa kuhimili misukosuko ya kiuchumi.

“Kwa uelewa wangu sekta ya fedha ambayo ni thabiti ni ile ambayo pale misukosuko ya kiuchumi inapotokea taasisi za fedha hususani mabenki yanakuwa na uwezo wa kuendelea kutoa huduma zote muhimu, kama malipo kwa wateja wake, utoaji wa mikopo, kuuza na kununua fedha za kigeni bila ya kutetereka."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news