NA GODFREY NNKO
MFUKO wa SELF (SELF Microfinance Fund) nchini umesema, hadi kufikia Desemba 31, 2023 walikuwa wametoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 324.51 ikiwa na kiwango cha mikopo chechefu chini ya asilimia 10 huku wakiweza kujiendesha kwa faida.
Afisa Mtendaji Mkuu wa mfuko huo, Mudith Cheyo ameyasema hayo leo Machi 11,2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wakiwemo waandishi wa habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
Mfuko wa SELF (SELF Microfinance Fund) ni zao la mradi wa Serikali ambao ulijulikana kama Small Entrepreneurs Loan Facility (SELF) ulioanzishwa mwaka 1999.
Aidha, ikiwa chini ya Wizara ya Fedha pia ni miongoni mwa taasisi na mashirika ya umma ambayo yanasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
TR ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.
Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa ofisi inayojitegemea kimuundo.
Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) ofisi ilikabidhiwa majukumu ya shirika hilo.
Kikao kazi cha leo ni mwendelezo wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kuzikutanisha taasisi na mashirika hayo ya umma na wahariri ili ziweze kuelezea walikotoka, walipo na wanapoelekea.
Dhamira ikiwa ni ili umma ambao ndiyo wamiliki wa taasisi hizo waweze kupata mwelekeo wake na kufahamu mafanikio yao.
Cheyo amesema kuwa, mikopo hiyo imechangia upatikanaji wa huduma za mikopo kwa wananchi wa kipato cha chini na cha kati nchini.
"Mikopo hiyo imeweza kuwafikia wanufaika wapatao 314,055 ambapo kati yao wanawake ni 166,449 sawa na asilimia 53 na waanaume 147,606 sawa na asilimia 47."
Afisa Mtendaji Mkuu huyo amefafanua kuwa, wanufaika hao wanatoka katika mikoa 30 ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.
Vile vile amefafanua kuwa, mfuko huo unafanya kazi nchi nzima kupitia matawi 12 ambayo yanajumuisha Mkoa wa Dar es Salaam ambalo linahudumia mkoa huo wenyewe na Mkoa wa Pwani.
Tawi la pili, Cheyo amsema ni la Zanzibar ambalo linahudumia Unguja na Pemba huku tawi la Kahama likihudumia mikoa ya Shinyanga, Tabora na Katavi.
"Na tawi la Morogoro linahudumia mkoa huo ambapo lile la Arusha linahudumia mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro. Tawi la Geita linahudumia mikoa ya Geita na Kagera huku Mtwara lilikihudumia mikoa ya Mtwara na Lindi."
Kwa upande wa tawi la Mwanza linahudumia mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu ambapo lile la Iringa linahudumia Mkoa wa Iringa, Ruvuma na Njombe huku Tanga ikihudumia Mkoa wa Tanga. Aidha, tawi la Mbeya linahudumia mikoa ya Mbeya, Rukwa na Songwe. Huku lile la Dodoma likihudumia Dodoma yenyewe na Shinyanga.
Pia,amesema Mradi wa SELF ulikuwa ni miongoni mwa programu za Serikali zinazotekeleza jukumu la kupunguza umaskini kwa niaba ya Serikali ambayo ilifadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).
Amesema, mradi ulilenga katika kuongeza mchango wa biashara ndogo za kati, katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini na kuimarisha tasnia ya mikopo midogo midogo nchini Tanzania.
Ni kupitia Mfuko wa Mkopo wa Jumla kwa Taasisi Ndogo za Fedha zinazostahiki (MFIs), kuimarisha uwezo wa kushirikiana MFIs kupitia mafunzo na usaidizi wa kitaasisi na kukuza na kuhamasisha uundwaji wa MFIs mpya za msingi nchini.
TEF
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatius Balile, Mjumbe wa Kamati Tendaji wa jukwaa hilo, Salim Said amesema kuwa, mfuko huo una nafasi kubwa ya kuweza kuboresha ustawi wa biashara za wananchi wenye kipato cha chini na cha kati.
Said amesema kuwa, ili mfuko uweze kuhudumia idadi kubwa ya watu ni jambo jema kuendelea kujitangaza na kutoa elimu kuhusu masuala yahusuyo fedha kwa wananchi hapa nchi waweze kutumia fursa zilizopo katika mfuko kujiendeleza.
Tags
Habari
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Ofisi ya Msajili wa Hazina
SELF Microfinance Fund
TEF Tanzania