Serikali kutumia bilioni 35 ujenzi jengo pacha TGC jijini Arusha, udahili kufikia 450 kwa mwaka

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Madini inatarajia kutumia shilingi bilioni 35 kujenga jengo pacha la Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) jijini Arusha, ambalo litasaidia kuongeza udahili kutoka wanafunzi 180 hadi 450 kwa mwaka.
Hayo yamebainishwa leo Machi 22,2024 jijini Arusha na Kaimu Mratibu wa kituo hicho, Mhandisi Ally Maganga wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu mradi wa ujenzi wa jengo hilo.

Mhandisi Maganga amesema, jengo hilo litakuwa na miundombinu mbalimbali ikiwemo madarasa, makumbusho, masoko ya madini ya vito, karakana za uongezaji thamani madini, maabara za madini ya vito na bidhaa za usonara, ofisi na mabweni ya wanafunzi.
Amesema, jengo hilo litakuwa mahsusi kwa utoaji wa mafunzo ya kuongeza thamani madini ya vito,minada ya madini ya vito na maonesho ya madini.

Mhandisi Maganga ameongeza kuwa, jengo litatimiza ndoto kubwa ya Serikali ya Tanzania kwa kulifanya eneo hili kuwa kitovu cha madini ya vito barani Afrika, hii ni kutokana na wingi wa rasilimali madini ya vito yaliyopo nchini.
Kuhusu miundombinu ya jengo hilo,Mhandisi Maganga ameeleza kuwa, ndani ya jengo hilo pacha kutakuwa na ofisi za Tume ya Madini pamoja na biashara ya minada ya madini ya vito ambayo yatasaidia kuleta fedha za kigeni nchini.

Akielezea kuhusu hali ya teknolojia ya uthaminishaji, Mhandisi Maganga amesema kuwa,bado nchi za Afrika zina changamoto kubwa ya teknolojia ya kusanifu madini, hivyo TGC itakuwa mkombozi mkubwa kwa wadau mbalimbali wa madini ya vito na metali hususani katika kuchakata na uthaminishaji.
Mradi huu unatarajia kukamilika ndani ya miaka miwili ijayo baada ya taratibu zingine kukamilika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. This comment has been removed by a blog administrator.

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news