NA GODFREY NNKO
SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha imekuwa ikitekeleza jukumu muhimu katika juhudi za kuimarisha sekta ya fedha kulingana na Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha 2020/21-2029/30.
Hayo yamebainishwa leo Machi 7, 2024 jijini Arusha na Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Hamad Hassan Chande (MB) wakati wa Kongamano la 21 la Taasisi za Fedha linaloendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Katika kongamano hilo linafanyika kwa siku mbili kuanzia leo Machi 7 hadi 8, mwaka huu huku likiongozwa na kauli mbinu isemayo “Kuimarisha Ustahimilivu wa Sekta ya Fedha Nyakati za Changamoto za Kiuchumi”,Mheshimiwa Chande amesema kuwa,
Wizara ikiwa kama msimamizi wa sera za kiuchumi, inashirikiana kwa karibu na wadau wa sekta ya fedha kutekeleza hatua zinazosaidia kuimarisha sekta ya fedha kwa kutunga na kutekeleza sera zinazoboresha mazingira ya udhibiti.
Pia, kuimarisha mfumo wa usimamizi wa vihatarishi, na kukuza uwezo ndani ya sekta ya fedha. "Kama alivyosema Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Emmanuel Tutuba), sekta ya fedha ya Tanzania imeonyesha uhimilivu katika kupambana na changamoto za uchumi wa dunia za hivi karibuni.
"Uimara wa sekta ya benki umesaidiwa na uwiano mzuri wa mtaji na ukwasi ambao ulikuwa juu ya mahitaji ya chini ya udhibiti."
Mheshimiwa Chande amesema, ufanisi huo unajionyesha katika ukuaji wa rasilimali (assets), hasa mikopo kwa sekta binafsi, ambayo ilikua kutokana na teknolojia za kifedha za hali ya juu na hatua zilizochukuliwa na Serikali na Benki Kuu ya Tanzania kuimarisha uchumi.
Amesema, mikopo hatarishi pia imebakia katika viwango vya chini, kama inavyoonekana katika kupungua kwa mikopo chechefu ambayo ipo chini ya kikomo cha asilimia 5 ya mikopo yote.
Pia,ongezeko la faida katika sekta ya benki limeongeza uimara wa kuhimili changamoto mbalimbali katika sekta hii.
"Masoko ya fedha na mitaji yalibaki kuwa imara na thabiti, na hivyo kuongeza ushiriki wa wawekezaji wa ndani.
"Sekta ya bima pia iliweza kuhimili changamoto kwa kuwa na mtaji na ukwasi wa kutosha, kama inavyojionyesha kwa ongezeko la malipo kamili na faida. Ufanisi huu mzuri pia ulionekana vilevile katika sekta ya hifadhi ya jamii, ambayo ilikuwa imara, kwa kuongezeka kwa mali na uwezo wa kutekeleza majukumu yake."
Kuhusu huduma jumuishi za fedha,Mheshimiwa Chande amesema, vilevile kuna mafanikio makubwa hasa kwenye ongezeko la upatikanaji na matumizi ya huduma rasmi za kifedha kama ilivyoonyeshwa kwenye matokeo ya utafiti wa FinScope wa mwaka 2023.
"Utafiti huu ulionyesha kuwa upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha nchini uliongezeka kutoka asilimia 86 mwaka 2017 hadi asilimia 89 mwaka 2023.
"Pia utafiti ulionyesha matumizi ya huduma rasmi za kifedha yaliongezeka kutoka asilimia 65 hadi asilimia 76.
"Mafanikio haya kwa kiasi kikubwa yalichangiwa na uwepo wa huduma za kifedha za kielektroniki, kuongezeka kwa uelewa wa wananchi juu ya bidhaa na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi za fedha nchini, na ushirikiano imara kati ya wadau wa kifedha wa umma na binafsi.
"Wizara inakusudia kuendelea kushughulikia masuala yanayohusiana na elimu ya kifedha na ubora wa huduma za kifedha nchini, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wake kwa gharama nafuu.
"Ninaamini kwamba hekima, uzoefu wetu, na utayari wetu wa kujitoa unahitajika kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa kifedha nchini ili uwe wenye nguvu na imara zaidi.
"Tunashukuru tumepata watoa mada mahiri na wenye weledi kutoka ndani na nje ya nchi ambao wapo tayari kutupatia uzoefu wao."
Mheshimiwa Chande amesema, Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika mapinduzi ya malipo ya huduma na bidhaa kwa kutumia simu za mikononi na benki za kidigitali.
Amesema, tayari mamilioni ya Watanzania wananufaika na upatikanaji wa huduma za kifedha zinazotolewa kwa njia ya simu kwa urahisi.
"Kuongezeka kwa huduma za kifedha zinazotolewa kwa njia ya simu kumeboresha kwa kiasi kikubwa namna ya kufanya na kutuma miamala ya kifedha, hivyo kuwawezesha wananchi na wafanyabiashara kusimamia fedha zao kwa usalama na urahisi."
Pia, Mheshimiwa Chande amempongeza Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba na taasisi washirika kwa kutengeneza Mfumo wa Taifa wa Malipo ya Papo kwa Papo (TIPS) ambao umezindua leo.
"Kama ilivyoelezwa na Gavana, Mfumo huu utawezesha uhamishaji wa fedha papo kwa hapo kati ya watoa huduma mbalimbali wa mifumo ya malipo, ikijumuisha benki na watoa huduma wa pesa kwa njia ya simu.
"Inategemewa mfumo huu utasaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwa watoa huduma na gharama za miamala kwa watumiaji,"amefafanua Mheshimiwa Chande.