DODOMA-Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa, Serikali kupitia Tume ya Madini itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini kama mkakati wa kuhakikisha mchango wao kwenye Sekta ya Madini unaendelea kukua sambamba na kuzalisha ajira zaidi.
Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo Machi 18, 2024 kwenye kikao cha sita cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma ambacho kimeshirikisha Wakurugenzi, Mameneja, Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, watumishi na wageni waalikwa kutoka TUGHE, na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Amesema kuwa, mchango wa wachimbaji wadogo kwenye mapato yatokanayo na Sekta ya Madini umeendelea kukua kutoka asilimia tano (5) hadi asilimia arobaini (40) Mwaka 2022/2023 na kusisitiza kuwa Tume ya Madini itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa wachimbaji wadogo sambamba na kutatua changamoto mbalimbali.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini, Mhandisi Samamba amesema kuwa ni pamoja na ongezeko la ukusanyaji wa maduhuli kutoka shilingi bilioni 213.3 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17 hadi shilingi bilioni 677.7 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023.
“Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 kama Tume ya Madini tulipewa lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 822 na kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 677.7 ikiwa ni (82.45%) na katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 tumepewa lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 882 ambalo ninaamini kabisa tutalivuka,” amesema Mhandisi Samamba.
Mhandisi Samamba ameendelea kusema kuwa siri ya mafaniko kwenye ukusanyaji wa maduhuli ni pamoja na uzalendo na ubunifu wa watumishi wa Tume ya Madini Makao Makuu, Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, Maafisa Migodi Wakazi na ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa Wizara ya Madini.
Ameendelea kueleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini 42 na vituo vya ununuzi wa madini 100 nchini, ongezeko la utoaji wa leseni za madini kutoka leseni 5094 katika mwaka wa fedha 2018/2019 hadi leseni 9642 katika mwaka wa fedha 2022/2023, kudhibiti utoroshaji wa madini na kupungua kwa ajali kwenye migodi ya madini kutokana na kaguzi zinazofanywa mara kwa mara kwenye shughuli za uchimbaji wa madini sambamba na kutolewa kwa elimu.
Amefafanua mafanikio mengine kuwa ni pamoja na ongezeko la ushiriki wa kampuni za kitanzania kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi kutokana na maboresho ya kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini.
Pia, amesema hadi kufikia mwaka 2022 asilimia 86 ya bidhaa na huduma zinatolewa na kampuni za kitanzania kwenye kampuni kubwa za uchimbaji wa madini huku asilimia 14 zikitolewa na kampuni za nje ya nchi kupitia kibali maalum.
Ni kinachotolewa na Tume ya Madini na kwa upande wa ajira katika migodi ya madini asilimia 97 ni watanzania huku raia wa kigeni wakiwa ni asilimia (3) tatu.
“Mchango wa Sekta ya Madini kweye Pato la Taifa uliongezeka kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017 hadi asilimia 9.1 mwaka 2022; tumejipanga kuhakikisha tunavuka lengo lililowekwa la asilimia 10 kabla ya mwaka 2025,” amesema Mhandisi Samamba.