PWANI-Kikao kazi cha Ofisi ya Msajili wa Hazina na wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika ambayo Serikali inamiliki hisa chini ya asilimia 50 kimefikia tamati, huku Serikali ikitoa maelekezo.
Kikao hicho cha siku tatu kimefanyika mjini Kibaha mkoani Pwani ambapo Ofisi ya Msajili wa Hazina iliwaketisha pamoja viongozi hao ili kuzungumza nao na kuwakumbusha matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akifunga kikao hicho Machi 15, 2024 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Professa Kitila Mkumbo ameziagiza bodi hizo zinazoiwakilisha Serikali kwenye mashirika zenye hisa chache kusimamia kwa ukamilifu mashirika hayo kwa maslahi mapana ya Taifa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Professa Kitila Mkumbo (Mb), akizungumza alipokuwa akifunga rasmi kikao kazi cha siku tatu kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na wajumbe wa Bodi na wakurugenzi wa Mashirika ambayo Serikali inamiliki hisa chini ya asilimia 50, Machi 15,2024 Kibaha, mkoani Pwani.
Prof.Mkumbo amesema kuwa, yapo mambo ambayo Serikali inawataka viongozi hao kuhakikisha wanayasimamia ili kuleta tija kwa Serikali na Taifa kwa ujumla.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida akitoa neno kwa wajumbe wa mkutano huo alipokuwa akimkaribisha mgeni rasmi kufungua rasmi mkutano huo.
Waziri huyo ameeleza kuwa, moja ya mambo ambayo Serikali inatamani kuona yanafanyika kwa kampuni hizo ni kuona zinawekeza nchini kwani zipo hapa hapa.
Msajili wa Hazina,Nehemiah Mchuchu akizungumza alipokuwa akitoa neno la utangulizi kuelezea kilichofanyika katika siku tatu za Mkutano huo Kibaha mkoani Pwani.
“Mna nafasi ya kuhakikisha kwamba makampuni haya yanawekeza Tanzania na kuendana na mazingira ya hapa nchini.
“Utakuta kampuni kubwa kutoka nje imewekeza nchini, lakini mazingira yao na namna wanavyoendesha kampuni kama wapo kwao,”amesema Prof.Mkumbo.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Ofisi ya Msajili wa Hazina,Amon Nnko, akiwasilisha maazimio ya kikao hicho.
Pia,amewataka viongozi hao kuwa na tabia njema na kuona ujuzi na mbinu ambazo zinazotumika kuhakikisha kampuni zao zinafanikiwa.
Vile vile, Prof. Mkumbo amewataka viongozi hao kutoa mrejesho kwa Serikali ambayo wanaiwakilisha kwa kutoka taarifa za mambo mbalimbali katika makampuni yao.
“Serikali imeamua kuijenga na kuikuza sekta binafsi katika nchi yetu ili itusaidie, na ukiangalia makampuni mnayofanyia kazi mengi ni sekta binafsi, hivyo kusimamia na kufanya kazi kwa weledi ili kuisaidia Serikali kufikia malengo yake,”amesema Prof. Mkumbo.