Serikali yawekeza nguvu kubwa katika miundombinu ya barabara

NA GODFREY NNKO

KATIKA kipindi cha miaka mitatu (2021 -2024), Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imefanikiwa kukamilisha miradi 25 ya barabara yenye urefu wa kilometa 1,198.50.

Pia,katika kipindi hicho, jumla ya barabara 57 zenye urefu wa kilometa 3, 794.1 ziko hatua mbalimbali za utekelezaji.
Msemaji Mkuu wa Serikali,Mobhare Matinyi ameyasema hayo leo Machi 24,2024 jijijni Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarani.

“Kadhalika, miradi ya ujenzi wa madaraja makubwa nane imekamilika.

"Aidha, miradi mitano ya ujenzi wa madaraja inaendelea kutekelezwa na ipo katika hatua mbalimbali."

Matinyi amesema,miradi hiyo ni pamoja na mradi wa kielelezo wa ujenzi wa daraja la J. P. Magufuli (Kigongo – Busisi) mkoani Mwanza lenye urefu wa mita 3,200 kwenye Ziwa Victoria.

“Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza miradi ya viwanja vya ndege ambapo vitano vimekamilika, miradi nane inaendelea chini ya TANROADS.

"Miradi ya ujenzi wa viwanja vya ndege inayoendelea ni pamoja na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, ambacho kinajengwa kwa fedha za Serikali (GOT) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)."

Msemaji Mkuu wa Serikalu ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza bajeti ya uboreshaji miundombinu chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na kufikia jumla ya shilingi trilioni 2.53 katika kipindi cha miaka mitatu.

Amesema, fedha hizo zimewezesha ujenzi wa barabara za lami za kilomita 819.22 (tofauti na barabara za lami zilizo chini ya TANROADS) na hivyo kuongeza mtandao wake kutoka kilomita 2,404.90 hadi 3,224.12.

“Kwa upande wa barabara za changarawe, jumla ya kilomita 11,924.36 zimejengwa na kuongeza mtandao wake kutoka kilomita 29,183.36 hadi 41,107.52. Kumekuwa pia na ujenzi wa madaraja mengi nchini ikiwemo kutumia teknolojia ya mawe."

Matinyi amesema, TARURA imepokea wito wa Mheshimiwa Rais Dkt.Samia wa kuhakikisha sasa inatumia teknolojia mbadala.

Amesema,majaribio ya teknolojia ya ECOROADS yameonesha mafanikio makubwa ambapo kilomita 22 zilijengwa katika eneo korofi na teknolojia hiyo kuhimili changamoto za eneo hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news