Simba SC yalipiza kisasi kwa Jwaneng Galaxy mabao 6-0 hakuna mtu aliyezimia kama Yanga SC

NA GODFREY NNKO 

LICHA ya Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam kuichapa mabao 6-0 Jwaneng Galaxy FC kutoka nchini Botswana, hakuna mtu aliyezimia kama ilivyokuwa kwa watani zao Yanga SC.

Ikumbukwe Februari 24,2024 Afisa habari wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe alidaiwa kuanguka na kupoteza fahamu baada ya mchezo wao kumalizika huku timu yake ikiwa na ushindi wa goli nne dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria.

Kamwe alikumbana na hali hiyo wakati akishangilia ushindi huo kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ambapo alianguka na kupoteza fahamu.

Aidha,Kamwe alichukuliwa na kutolewa nje ya vyumba hivyo kisha kupelekwa hospitali huku akiendelea kupatiwa matibabu akiwa ndani ya gari la wagonjwa.

Katibu wa Madaktari wa Tiba za Wanamichezo nchini, Dkt. Juma Sufian alithibitisha tukio hilo. 

Mchezo huo wa Kundi D wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika ulipigwa Februari 24,2024 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

SIMBA SC

Aidha, leo kuanzia saa moja usiku Simba SC wameshuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Jwaneng Galaxy katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo huo ambao walisema ni fainali kwao hivyo ni wa kufa na kupona wameishinda kwa kishindo.

Ni baada ya mabao sita kuwekwa nyavuni na Said Ntibazonkiza dakika ya saba, Pa Omar Jobe dakika ya 14 akatupia lingine ambalo kabla ya kupoa Kibu Denis dakika ya 22 aligonga msumari mwingine.

Hadi kipindi cha kwanza kinatamatika Simba sC walikuwa na ushindi wa mabao 3-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kila upande kumvizia mwenzake ambapo, Clatous Chama dakika ya 76 aligonga msumari wa nne huku dakika ya 86 Ladaki Chasambi akiweka bao la tano ambalo limefuatiwa na Fabrice Ngoma dakika ya 89.

Hiyo ilikuwa ni ndoto ya kila Mwanasimba kuiona timu yake ikitinga robo fainali leo.

Awali, Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha alisema wanahitaji kushinda kwa ajili ya mashabiki wao ambao wamekuwa nao katika kipindi chote na wanastahili kupata furaha kwenye mchezo wa leo.

“Sisi tunatakiwa kushinda hatumuangalii mtu wala matokeo ya timu nyingine, hii ndio faida yetu, tunatakiwa kuwa imara tushinde kwa ajili ya mashabiki wetu na Watanzania wote wanaotusapoti,” alisema Benchikha.

Pengine hii ilikuwa ni mechi ya kisasi, kwani Oktoba 24, 2021 Simba SC walikutana na Jwaneng Galaxy katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na waliwafunga mabao 3-1 na kuwatoa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Kikosi cha Simba SC

Ayoub Lakred (36), Shomari Kapombe (12), Mohamed Hussein (15), Che Malone (20), Henock Inonga (29), Babacar Sarr (33), Kibu Denis (38), Fabrice Ngoma (6), Pa Omar Jobe (2), Said Ntibazonkiza (10), Clatous Chama (17).

Wachezaji wa akiba

Aishi Manula (28), Israel Patrick (5), Kennedy Juma (26), Edwin Balua (37), Mzamiru Yassin (19), Freddy Michael (18), Abdallah Hamisi (13), Luis Miqussone (11), Ladaki Chasambi (34).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news