NA GODFREY NNKO
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeendelea kurekodi mafanikio makubwa kupitia ongezeko la watalii na mapato chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Mussa Juma Kuji ameyasema hayo leo Machi 21, 2024 katika kikao kazi na wahariri wakiwemo waandishi wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
Katika kikao hicho, Kamishna Kuji ameelezea mafanikio yaliyopatikana katika Hifadhi za Taifa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2021 hadi 2024) ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
"Vilevile, nitoe pongezi kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuratibu programu hii muhimu ya kueleza kwa umma mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Kadhalika nitoe pongezi kwa wanahabari wote wa ndani na nje ya nchi kwa ushirikiano mnaoendelea kuutoa kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kuuhabarisha umma jitihada za uhifadhi zinazofanywa na TANAPA."
Amesema, mafanikio ya leo yanatokana na jitihada za makusudi zinazoendelea kufanywa na Rais Dkt.Samia ambazo zinaambatana na ushiriki wake wa moja kwa moja kwenye kukuza sekta ya uhifadhi wa wanyamapori na utalii ikiwemo ushiriki wake kwenye filamu maarufu ijulikanayo kama “Tanzania: The Royal Tour”.
"Filamu hii imeleta chachu kubwa katika ukuaji wa utalii hapa nchini. Tunampongeza sana Mhe. Rais kwa mchango wake huu katika sekta ya uhifadhi na utalii hapa nchini pamoja na kuendelea kuelekeza fedha katika sekta ya uhifadhi na utalii."
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, Kamishna huyo amesema, Filamu ya Tanzania, The Royal Tour ilifungua milango ya utalii na fursa za uwekezaji katika Hifadhi za Taifa hasa baada ya nchi kutoka kwenye athari za janga la UVIKO-19.
"Katika Hifadhi za Taifa kumekuwa na ongezeko la watalii wanaotembelea Hifadhi za Taifa mwaka hadi mwaka.
"Mfano katika mwaka 2018/2019 jumla ya watalii waliotembelea Hifadhi za Taifa walikuwa watalii 1,452,345 ikihusisha watalii wa ndani (719,172) na nje (733,173)."
Kamishna Kuji amesema, idadi hiyo ilianza kupungua mwanzoni mwa mwaka 2020 kutokana na janga la UVIKO-19 na kusababisha idadi ya wageni kupungua hadi kufikia watalii 485,827 katika mwaka 2020/2021.
"Kufuatia anguko hili la utalii, Serikali ya Awamu ya Sita ilichukua hatua mbalimbali katika kurejesha hali ya utalii kama ilivyokuwa hapo awali ikiwemo kutengenezwa kwa miongozo maalum (Standard Operating procedures - SOPs) ya kupokea na kuhudumia watalii, na pia kuruhusu upatikanaji wa chanjo ya UVIKO-19.
"Hili lilienda sambamba na utangazaji mahiri wa vivutio vyetu kupitia filamu ya Tanzania:The Royal Tour iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuzinduliwa 2022."
Amesema, kutokana na jitihada hizo za Mhe. Rais, mnamo mwaka 2021/2022 idadi ya watalii ilianza kupanda na kufikia watalii 997,873.
Kamishna Kuji amesema, hali ya kuimarika kwa utalii nchini iliendelea kupanda ambapo mwaka 2022/2023 idadi ya watalii waliongezeka na kufikia 1,670,437.
Aidha, kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Machi 19, 2024 idadi ya watalii 1,514,726 (wa ndani wakiwa 721,543 na wa nje wakiwa 793,183) wametembelea hifadhi za Taifa sawa na ongezeko la asilimia tano ikiwa ni zaidi ya lengo la kupokea watalii 1,387,987 (wa nje 827,713 na watalii wa ndani 726,676) katika kipindi husika.
Afisa Mawasiliano Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho kati ya TANAPA na wahariri chini ya uratibu wa ofisi hiyo leo.
Pia amesema, idadi ya watalii wanaotarajiwa kutembelea Hifadhi za Taifa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ni 1,830,081 (watalii wa nje 963,413 na watalii wa ndani 866,667).
Vilevile,Kamishna Kuji amesema, katika kipindi cha miaka mitatu kumekuwepo na ongezeko la siku za kukaa wageni kutoka wastani wa siku 1,749,194 katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia wastani wa siku 2,669,586 kufikia Februari 2024.
"Ongezeko hili limechangia ongezeko la mapato.Katika kipindi cha miaka mitatu, kumekuwepo na ongezeko la mapato kutoka shilingi 174,715,158,494 (2021/2022) hadi kufikia shilingi 337,424,076,896 (2022/2023) sawa na ongezeko la shilingi 162,708,918,402 ambayo ni asilimia 94."
Aidha, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 (Julai 2023 hadi Machi 19, 2024), Kamishna Kuji amesema, shirika limekusanya shilingi 340,101,108,465 ukilinganisha na matarajio ya kukusanya shilingi 295,466,811,506 mpaka Machi, 2024.
"Kiasi hiki (shilingi bilioni 340) ni ongezeko la shilingi 44,634,296,959 ambayo ni sawa na asilimia 15. Shirika lina matarajio ya kukusanya kiasi cha shilingi 382,307,977,497 hadi Juni 2024."
Kamishna Kuji amesema, mapato haya ya sasa yanazidi mapato ya shilingi 282,450,446,103 yaliyokusanywa mwaka 2018/2019 kabla ya janga la UVIKO-19 ambayo yalikuwa ndio kiwango cha juu cha mapato katika shirika.
Amesema, ongezeko hili la watalii na mapato linaenda sambamba na malengo ya Ilani ya Chama Chama Cha Mapinduzi ya 2020 hadi 2025 inayoelekeza idadi ya watalii nchini kufikia milioni 5 na mapato ya dola za kimarekani Bilioni 6 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ni taasisi ya umma ambayo ipo chini ha Wizara ya Maliasili na Utalii, lilianzishwa mwaka 1959 kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura ya 412 (National Parks Act Cap. 282) na marekebisho Na. 282 ya 2002 yenye dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yote yaliyotengwa kuwa Hifadhi za Taifa.
Maeneo ya Hifadhi za Taifa yanawakilisha kiwango cha juu kabisa cha uhifadhi wa wanyamapori nchini (highest conservation status of wildlife) ambapo hakuna shughuli zozote za kibinadamu zinazoruhusiwa kufanyika.
Hadi sasa Shirika linasimamia hifadhi za Taifa 21 zenye eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 96,908.88 ambalo ni sawa na asilimia 10.2 ya eneo lote la nchi. Aidha, TANAPA licha ya kuwa chini ya wizara pia, inasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.