WINDHOEK-Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewanoa watumishi wa Taasisi ya Hali ya Hewa Namibia.
Ni kwa kuwapatia mafunzo ya kuhakiki weledi wa wafanyakazi wote wanaofanya kazi za kutoa huduma za hali ya hewa katika viwanja vya ndege.
Mafunzo hayo yalifanyika katika ofisi za Hali ya Hewa jijini Windhoek nchini Namibia kuanzia Machi 4 hadi 18, mwaka huu.
Akizungumza wakati wa kufunga rasmi mafunzo hayo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Caesar Waitara ameishukuru Taasisi ya Hali ya Hewa Namibia kwa kuichagua Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuendesha mafunzo hayo.
Balozi Waitara amesema, pamoja na uwepo wa taasisi nyingi za hali ya hewa barani Afrika, TMA imepewa kipaumbele.
Aidha, alizitaka taasisi zote mbili kuongeza ushirikiano zaidi katika masuala mbalimbali kwa lengo la kunyanyua uchumi na maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa nchini kwetu ikiwa ni pamoja na kufunga miundombinu ya kisasa ya hali ya hewa.
"Mafunzo kwa watumishi kwa kuzingatia vigezo vya kitaifa na kimataifa, na kuweka mifumo wezeshi ya usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa urahisi kwa watumiaji wa taarifa hizo, pamoja na kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa huduma (QMS) na weledi wa wafanyakazi,”amesema Balozi Waitara.
Aidha, alieleza kuwa, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzoni kabisa kufanikisha kupata cheti cha ubora wa Kimatiafa cha ISO 9001:2015 katika utoaji wa huduma za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga.
Kupitia mafanikio hayo, Tanzania kupitia TMA imeweza kuzisaidia nchi zingine kama vile Nigeria, Libya, Saudi Arabia, Maldives na Lesotho katika masuala uanzishaji na utekelezaji wa mifumo ya utoaji huduma bora za hali ya hewa katika viwango vinavyotambulika kimataifa.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Hali ya Hewa Namibia, Bw. Elias Aiyambo, aliishukuru Serikali yake kwa kukubali maombi ya kufanya mafunzo hayo muhimu kwa nchi, vilevile aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha mafunzo na kuomba ushirikiano huo uendelee baina ya nchi hizi mbili.
Tags
Habari
Kimataifa
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
TMA Tanzania