TASAC yafafanua kuhusu kuzama boti ya MV LEGACY

DAR ES SALAAM-Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa taarifa kwa umma kuhusu tukio la kuzama kwa boti ya uvuvi MV LEGACY yenye namba ya usajili DS/L1175 inayomilikiwa na Yakoub Juma Khamis.
Ni boti yenye urefu wa mita 11 na upana wa mita 1.7 iliyopatiwa Cheti cha Usajili na Ubora na TASAC kufanya shughuli za uvuvi mnamo tarehe 06/03/2024.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 11,2024 na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu,Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).

"Mnamo tarehe 10/03/2024 majira ya 10:01 alasiri, Kituo chetu cha Kuratibu shughuli za Utafutaji na Uokoaji (MRCC) kilipokea taarifa ya kuzama kwa boti ya uvuvi MV LEGACY iliyotokea majira ya saa 9:50 jioni karibu na fukwe ya Coco Beach, Msasani, Wilaya ya Kinondoni mjini Dar es salaam ambayo ilikuwa na jumla ya mabaharia tisa (09) ikijumuisha Wavuvi sita (06), Mhandisi Mitambo mmoja (01) na Manahodha wawili (02).

"Kituo cha MRCC kilifanya jukumu lake la kisheria la kuratibu shughuli ya uokoaji kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi (Wanamaji) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kufanya juhudi za kufika eneo la tukio na kufanya zoezi la uokoaji. Watu wote tisa wamefanikiwa kuokolewa na wanaendelea vizuri kiafya bila ya kuwa na changamoto yoyote.

"Boti hiyo ambayo ilikuwa katika majaribio ya kiufundi baada ya matengenezo ya mifumo ya uvuaji samaki kwa kukokota (Trawling), ilianza majaribio majira ya saa 3:00 asubuhi ikitokea maeneo ya Tandavamba, Kivukoni na kufanya majaribio ya kuvua samaki wakizunguka katika maeneo yenye maji mafupi karibu na eneo la daraja jipya la Tanzanite (Upanga) hadi Coco Beach (Oysterbay).

Ilipofika majira ya saa 9:50 Alasiri wakati nahodha anabadilisha uelekeo wa boti kuelekea upande wa kulia ndipo kamba moja ya upande wa kushoto ikakatika na kusababisha uzito kelemea kwenye kamba ya upande wa kulia na ndipo uzito ulipohama ghafla na kuilazimisha boti kunywa maji upande wa kulia kisha kuzama.

"TASAC inaendelea kutoa rai kwa wamiliki na waendeshaji wa vyombo majini kuzingatia
Sheria na Kanuni za udhibiti usafiri majini na kuhakikisha muda wote wanavalia majaketi
okozi ili kujiepusha na maafa yanayoweza kusababishwa na tukio la ajali,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo ya TASAC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news